SERIKALI KUENDELEA NA UREJESHAJI WAKIMBIZI WA BURUNDI KWA HIYARI

0

Serikali ya Tanzania imethibitisha azma yake ya kuendelea kushirikiana na Serikali ya Burundi, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Wakimbizi Duniani (UNHCR) kuwarejesha kwa hiari yao wakimbizi kutoka nchi ya Burundi waliopo Tanzania kama sehemu ya jitihada za kusaidia kurejesha maisha ya kawaida kwa wakimbizi hao

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo katika Mkutano wa 25 wa Pande Tatu Kuhusu Urejeshaji wa Hiari wa Wakimbizi Kutoka nchini Burundi wanaohifadhiwa Tanzania uliofanyika jijini Bujumbura Disemba 19, 2024.

Mhe. Sillo amesema kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) na Serikali ya Burundi katika kuhamasisha wakimbizi wa kutoka Burundi kurejea kwa hiari nchini kwao.

“Ni jukumu letu kusaidia wakimbizi kurudi nyumbani kwa heshima na usalama. Tutaendelea na juhudi za kuwahamasisha, huku tukishirikiana kwa karibu na pande zote husika”. Amesema Sillo

Naibu Waziri Sillo amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na UNHCR itaendelea kutoa elimu kwa wakimbizi kuhusu fursa zinazowasubiri nyumbani kwao sambamba na hilo Serikali ya Tanzania imependekeza kwa Serikali ya Burundi kuanzisha maeneo tengefu ambapo miundombinu ya huduma za kijamii zitaboreshwa zaidi katika maeneo hayo ili kutoa motisha zaidi kwa Wakimbizi kurejea nyumbani.

Hata hivyo, Mhe Sillo alieleza kuwa Serikali ya Tanzania haifurahishwi na na kasi ya urejeaji licha ya jitihada kubwa sana zilizofanyika za uhamasishaji jambo ambalo linatulazimu kuwa wabunifu zaidi na kufikiria njia mbadala ili kuhakikisha wakimbizi walioko wanapata suluhisho la kudumu. Pamoja na hilo Serikali imekubali kuendelea na uhamasishaji kwa mwaka mmoja ili kuendelea kutathimini mwenendo wa zoezi hilo.

Pia, Mhe Sillo alieleza kuwa, pamoja na kuendelea na uhamasishaji wakimbizi wa Burundi kurejea katika nchi yao, kwa mwaka 2025, Serikali ya Tanzania itafanya zoezi muhimu la tathimini ya kina inayolenga kutoa suluhisho la kudumu kwa wakimbizi wote wa Burundi wanaohifadhiwa Tanzania (Comprehensive Protection and Solution Based Assessment). Zoezi hilo litafanywa kwa kushirikiana na UNHCR pamoja na wadau wote muhimu hivyo, alihimiza Jumuiya ya Kimataifa, wadau na wafadhili wa masuala ya wakimbizi kuangalia namna wanavyoweza kuisaidia Serikali ya Tanzania kufiki azma hiyo.

Mkutano huo umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi akiwemo Naibu Katibu Mkuu, Dr. Maduhu Kazi na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi Sudi Mwakibasi pamoja na Maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *