DKT. SERERA: FANYENI KAZI KWA USHIRIKIANO
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Suleiman Serera ametoa wito kwa Watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano, weledi na uadilifu katika utendaji kazi wa kila siku na utoaji huduma kwa umma hususani Wafanyabiashara ili kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuendeleza Sekta ya Viwanda na Biashara na kujenga uchumi imara wa Viwanda.
Dkt. Serera ameyasema hayo Disemba 19, 2024 mara alipowasili na kupokelewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Needpeace Wambuya pamoja na Menejimenti na Watumishi katika Ofisi ya Wizara hiyo zilizopo Mtumba Dodoma.
Aidha, Aliwaasa Watumishi hao kutimiza majukumu yao kikamilifu kwa kushirikiana bila kujali kada zao kwa kuwa kila Mtumishi ana majukumu yake mahususi yanyayochangia katika kuendeleza Sekta ya Viwanda na Biashara ambayo ina mchango mkubwa katika ujenzi wa Uchumi wa Taifa
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Needpeace Wambuya, amemuahidi Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa Wizara hiyo pamoja na Watumishi wake iko tayari kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na kwa ushirikiano katika utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara ili kuhakikisha inaendeleza sekta hiyo muhimu katika kuongeza ajira, Pato la Taifa na uchumi kwa ujumla
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Rasilimali watu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bi. Veronica Nchango akiongea kwa niaba ya Watumishi hao alisema wanamkaribisha Naibu Katibu Mkuu huyo kwa moyo mmoja na wako tayari kufanya naye kazi kwa ushirikiano ili kutimiza malengo tarajiwa yaliyowekwa.