PROF. LIPUMBA ASHINDA TENA UENYEKITI CUF
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa Prof. Ibrahim Lipumba ametetea kwa mara nyingine tena nafasi yake ya Uenyekiti baada ya kuibuka Mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa Chama hicho akipa kura 216 kati ya kura halali 592 zilizopigwa huku anayemfuatia Hamad Masoud akipata kura 181.
Uchaguzi huo ulikuwa na Wagombea 9 akiwemo Ali Juma Khamis ambaye alijitoa dakika za mwisho, Mgombea wa pili ni Athman Kanali aliyepata kura 5, Hamadi Hamadi kura 181, Juma Shaban kura 6, Maftaha Abdallah Nachuma kura 102, Wilfred Lwakatare kura 78, Ngaitile Siwale kura mbili na Chifu Lutalosa Yemba kura mbili .
Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi CUF Taifa amesema “Kwa matokeo haya niliyonayo na kwa nafasi yangu ya Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi namtangaza Ibrahim Lipumba kuwa ndiye Mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa uchaguzi wa CUF, Ndugu zangu kwa Mgombea ambaye hajaridhika na matokeo tunayo Kamati ya Rufani anakaribishwa kuwasilisha rufaa yake kwa Kamati hiyo”
Prof. Lipumba amekuwa Mwenyekiti wa CUF kwa miaka 25 sasa tangu aliposhika nafasi hiyo mwaka 1999.