WAZIRI ULEGA AKAGUA MIRADI YA BRT, AAGIZA KAZI IFANYIKE USIKU NA MCHANA.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Balozi, Mhandisi, Aisha Amour kuwasimamia kikamilifu Wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka jijini Dar es Salaam kwa kufanya kazi usiku na mchana ili ikamilike kwa wakati na kupunguza changamoto ya msongamano wa magari katika jiji hilo.
Aidha, Ulega ametoa siku tatu kwa Mkandarasi wa Kampuni ya Sichuan Road and Bridge Group anayetekeleza upanuzi barabara ya Ubungo – Kimara kuongeza idadi ya watalaam na vibarua pamoja na kufunga taa nyakati za usiku ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
Ulega ametoa maelekezo hayo leo Disemba 15, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) na kuagiza ujenzi wa miundombinu hiyo uende sambamba na uwekaji wa Taa za Barabarani kwa ajili ya Ulinzi na Usalama na kupendezesha mandhari ya jiji hilo.
Waziri Ulega amekagua upanuzi unaoendelea katika mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Kwanza inayoanzia Ubungo hadi Kimara na kutoridhishwa na kasi ya maendeleo yake ambao umefikia asilimia 26 tofauti na matakwa ya mkataba unaomtaka mkandarasi kufikia asilimia 52.
“Ni ukweli usiopingika kwamba kipande hiki cha kutoka Ubungo – Kimara ni kisumbufu mno, foleni ni kubwa sana, watu wanateseka na kupata adha hivyo Mkandarasi fanya kazi usiku na mchana umechelewa sana na hatutaki kuona watu wanataabika hapa”, amesisitiza Waziri Ulega.
Waziri huyo amesisitiza kutowavumilia Wakandarasi wazembe wanaoshindwa kutekeleza miradi kwa wakati na ameahidi kuwachukulia hatua za kimkataba na wengine kutopatiwa kazi nyingine za ujenzi hapa nchini.
Vilevile, Waziri Ulega ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi miundombinu ya BRT Awamu ya Tatu inayoanzia katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Gongo la Mboto unaotelelezwa na Mkandarasi Sinohydro kwa gharama ya Shilingi Bilioni 231 ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika Mwezi Machi 2025.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Ukonga na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utelelezaji wa ujenzi wa mradi wa BRT Awamu ya Tatu kwa kuwa ukikamilika utaongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi wa Ukonga na kupunguza muda wa usafiri kutoka saa mbili kwa magari ya kawaida hadi dakika 45 na kwa mabasi ya mwendo kasi dakika 30.
Kwa upande wake, Msimamizi wa miradi ya ujenzi wa BRT kutoka TANROADS, Mhandisi Frank Mbilinyi ameeleza kuwa Mradi wa Usafiri wa Haraka wa Mabasi (BRT)) ulibuniwa mwaka 2004 chini ya Halmashauri ya Jiji kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari barabarani Jijini Dar es Salaam ambapo Mpango Mkakati wa mradi huo umeainisha awamu sita za barabara kujengwa.