MUHTASARI WA YALIYOSEMWA KWENYE UZINDUZI WA MADINI YA VITO MIRERANI DESEMBA 14, 2024

0

WAZIRI WA MADINI, MHE. ANTHONY MAVUNDE

Nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nia yake ya dhati ya kuiwezesha Sekta ya Madini ambapo mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kuimarika.

Kutokana na maboresho ya Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja uanzishwaji wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini makusanyo ya maduhuli yameongezeka kutoka shilingi bilioni 161 mwaka 2015/2016 hadi kufikia shilingi bilioni 753 mwaka 2023/2024. Katika mwaka wa fedha 2024/2025 Wizara ya Madini imepanga kukusanya shilingi Trilioni Moja. Kuanzia kipindi cha Julai 01 hadi Desemba 01, 2024 kiasi cha shilingi bilioni 434 kimeshakusanywa.

Napenda kuwashukuru na kuwapongeza wote mliohusika katika kufanikisha urejeshwaji wa minada ya madini ya vito hapa nchini. Uwepo wa minada hii ni hatua muhimu ya kuhakikisha bei halisi ya madini ya vito inapatikana kwa njia ya ushindani na uwazi.

Urejeshwaji wa minada ya madini ya vito ni dhamira ya Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusimamia Sekta ya Madini kwa weledi ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika na rasilimali madini.

Uwepo wa minada hii utasaidia kufungamanisha Sekta ya Madini na Sekta nyingine za uchumi mfano viwanda, biashara na utalii na hivyo kutimiza malengo ya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya madini ya vito barani Afrika na Duniani kwa ujumla.

Uwepo wa minada hii utawanufaisha wadau na Taifa kwa ujumla kwa kuzingatia kuwa, Tanzania imejaliwa madini mengi ya vito, pamoja na kusisimua na kuchagiza biashara ya madini ya vito hapa nchini kwa ufanisi zaidi.

Serikali itaendelea kuimarisha masoko ya madini ya vito kwa kuendesha minada kwa uwazi kupitia mfumo wa kielektroniki uliojengwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Madini na Wizara ya Fedha kupitia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).

Wizara pia imepanga kuratibu minada ya mara kwa mara katika maeneo yenye uzalishaji wa madini ya vito nchini ili kurahisisha biashara ya madini na kuongeza ushiriki wa wadau kutoka katika Mikoa ya kimadini. Kwa kupitia mikakati hii, Wizara itaendelea kutoa fursa kwa wachimbaji na wadau wote kushiriki kikamilifu katika mchakato wa minada.

Kutokana na uanzishwaji wa minada ya madini ya vito, kumekuwa na kauli za upotoshaji kwamba Serikali itachukua madini yenu. Napenda kuwahakikishia kuwa, Serikali ina nia nzuri katika biashara hii na kila mtu atapata stahiki yake. Aidha, madini ambayo hayatauzika wakati wa minada, yatarudishwa kwa wamiliki

Serikali inaendelea kutoa wito kwa wadau wa ndani na wa kimataifa kushiriki kikamilifu katika minada ya madini ya vito, kama Tanzanite, ili kuongeza ushindani wa bei, kuvutia wanunuzi wa kimataifa, na kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya taifa letu.

Serikali itaendelea kuboresha miundombinu hasa ya barabara kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa madini sambamba na kuboresha huduma za jamii kama vile zahanati na shule kwa jamii inayoishi karibu na migodi ya madini.

Kama mkakati wa kuendelea kutangaza madini ya vito hasa Tanzanite, Serikali itaendelea kufanya minada mbalimbali sambamba na ushiriki katika maonesho ya kimataifa lengo likiwa ni kupandisha hadhi ya madini haya.

Serikali ina mpango wa kujenga mji (Tanzanite Smart City) katika eneo la Mirerani mkoani Manyara ambapo mikutano ya kimataifa ya madini itakuwa inafanyika sambamba na mikoa mingine kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa miji kwa ajili ya mikutano na biashara za kimadini

Ili kuhakikisha kila mdau anashiriki katika minada hii, kutakuwepo pia na minada ya wafanyabiashara wadogo wa madini.

NAIBU KATIBU MKUU WA WIZARA YA MADINI, MSAFIRI MBIBO

Kabla ya kuanza kwa minada ya madini kulikuwepo na maonesho ya minada iliyoanzishwa na Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) kuanzia mwaka 1992 hadi mwaka 1998 ambapo baadaye ulianzishwa mnada wa madini wa vito uliojulikana kama Arusha Gem Fair mwaka 2012 uliosimamishwa na Serikali Desemba, 2017 ikiwa ni mkakati wa kuangalia namna bora ya kufanya maboresho ya kuhakikisha nchi inanufaika na uwepo wa madini ya vito.

Kupitia mnada huu idadi ya washiriki waliosajiliwa ni 195 ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara wadogo wa madini 120, wafanyabiashara wakubwa wa madini 59, waongezaji thamani madini 7 na wachimbaji 7.

Jumla ya kilogramu za madini ya vito 184.06 zenye thamani ya shilingi bilioni 3.1 zimepokelewa kwenye mnada.

MWENYEKITI WA TUME YA MADINI, JANET LEKASHINGO
Nawapongeza wadau wote wa madini walioleta madini yao hapa kwa ajili ya mnada. Ninawaomba wadau wote kuendelea kushiriki katika mnada huu unaofanyika kwa njia ya kielektroniki ambao ni endelevu

MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI MHE. KILUMBE NGÉNDA

Naipongeza Wizara ya Madini kwa kuweka nguvu kubwa kwenye utafiti wa madini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na kuwezesha wachimbaji kuchimba bila kupoteza mitaji.

Kamati itaendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara lengo likiwa ni kuhakikisha mchango wa Sekta ya Madini unakua na kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025

MBUNGE WA SIMANJIRO MHE. CHRISTOPHER OLE SENDEKA

Naipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kupania kuleta mapinduzi ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini, kuhakikisha dhahabu inanunuliwa kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hivyo kuendelea kuimarisha uchumi wa nchi.

Ninashauri Serikali kuendelea kutilia mkazo wa biashara ya madini ya vito kuendelea kufanyika katika mji wa Mirerani wakati ujenzi wa Soko la Madini Mirerani ukiendelea.

MKUU WA MKOA WA MANYARA, MHE. QUEEN SENDIGA

Ninaipongeza Serikali kwa urejeshaji wa minada ya madini ambayo ilikuwa imesimama kwa miaka sita

Minada hii italeta manufaa makubwa kwa nchi ikiwa ni pamoja na kukuza kipato kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini, serikali kupata mapato, kuimarisha ubora wa madini ya vito na kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini.

Ninampongeza Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde kwa kuendelea kuipaisha Sekta ya Madini sambamba na kuitangaza ndani na nje ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *