BENKI YA TADB ILIVYOCHANGIA KASI YA UZALISHAJI WA SAMAKI PWANI

0


Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imefanikiwa kuiwezesha mtaji Kampuni ya Ufugaji wa Samaki Tanlapia na kufanikiwa kupiga hatua ya uzalishaji wa samaki aina ya sato kutoka tani tano (5) hadi kufikia tani 35 kila mwezi pamoja na kutoa ajira 116 jambo ambalo limeleta tija kwa Taifa.

Akizungumza Disemba 13, 2024 Mkoani Pwani wakati Wanahabari walipotembelea mradi wa kimkakati wa ufugaji wa samaki wa Kampuni ya Tanlapia uliopo Kata ya Nia Njema, Wilaya ya Bagamoyo, Meneja wa Kanda ya Mashariki Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Bw. Michael Madundo, amesema kuwa Tanlapia ni mradi wa kimkakati ambapo benki ya TADB wanajivunia kutokana umeleta mafanikiwa makubwa.

Bw. Madundo amesema kuwa mradi huo wa ufugaji wa samaki unatumia teknolojia ya kisasa ambayo inatumia   maji kidogo na kuzalisha samaki wengi na kuleta ufanisi katika utendaji.

“Mradi huu unasaidia kutekeleza majukumu ya Serikali kwa kuongeza utoshelezaji wa chakula nchini, kwani mahitaji ya chakula nchini hasa samaki kwa mwaka tani  laki tatu” amesema Bw. Madundo.

Bw. Madundo amefafanua kuwa ulaji wa samaki nchini upo chini ya wastani kwani mtu mmoja anakula kilo sita hadi saba kwa mwaka badala ya kula kilo 20 kwa mwaka.

”Bado hatupati protini ya kutosha, hivyo mradi huo unavyotekelezwa unaweza kutusongeza katika malengo ya Taifa kwa kuongeza utoshelezi wa chakula na kuhakikisha wananchini wanapata virutubisho vya kutosha” amesema Bw. Madundo.

Amesema kuwa mradi umeajiri wanawake pamoja na vijana, huku akieleza kuwa kadri muda unavyozidi kwenda wataendelea kutoa ajira hasa kwa wananchi wanaoishi katika Wilaya ya Bagamoyo.

Meneja wa Uzalishaji Kampuni ya Tanlapia Bi. Farida Buzohera, ameishukuru Benki ya TADB kuwa kuwawezesha kiuchumi kwa kufanya maboresho ya miundombinu ya uzalishaji wa samaki.

Bi. Buzohera amesema kuwa kupitia uwezeshaji huo wamefanikiwa kupiga hatua na kuzalisha tani 35 za samaki kila mwezi, huku akieleza  mpaka kufikia mwaka 2025 wanatarajia kuzalisha tani 100 kwa mwezi.

Amesema kuwa mafanikio waliopata yametokana na ushirikiano mkubwa kutoka benki ya TADB kwani awali walikuwa wanazalisha kiasi kidogo cha samaki tofauti na sasa.

“Kuna upungufu wa samaki Ziwa Victoria, Bahari ya India, hivyo kuna ukosefu mkubwa wa protini kwa ujumla nchini, hata ukifikia uzalishaji wa tani 100 hatuwezi kukizi mahitaji ya wananchi wote, tunaendelea kuongeza idadi ya uzalishaji kila mwaka” amesema Bi. Buzohera.

Amesema kuwa Tanlapia inafanya kazi kubwa ya uzalishaji wa vifaranga vya samaki, ukuzaji pamoja na kuuza wa samaki wakubwa, huku akifafanua kuwa samaki wanaozalisha na kuingia sokoni ni wakubwa ambapo watatu sawa na kilo moja.

“Uzalishaji wa samaki mpaka inamfikia mraji inachukua muda wa miezi tisa, na tunauza kwa bei rafiki lengo ni kuhakikisha kila mtazania anapata protini kupitia samaki, na soko kubwa lipo Mkoa wa Pwani pamoja na Dar es Salaam” amesema  Bi. Buzohera.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *