WAZIRI NDEJEMBI AMREJESHEA MWANANCHI ENEO LAKE KOROGWE
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi, amechukua hatua ya kumrejeshea Bw. Rajabu Risasi, mkazi wa Korogwe, mkoani Tanga eneo lake baada ya kuhangaika kwa muda mrefu kufuatia kudhulumiwa eneo hilo.
Akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Korogwe, Waziri Ndejembi alieleza kuwa malalamiko ya Bw. Risasi yalifikishwa kwake na kufanyiwa uchunguzi wa kina na baada ya kupitia nyaraka za umiliki, ilithibitika kuwa Bw. Risasi imegundulika kuwa alikuwa mmiliki halali wa eneo hilo tangu mwaka 1999.
“Serikali inasimama na haki, kupitia nyaraka, nimejiridhisha, Bw. Rajabu Risasi arejeshewe eneo hili ili haki yake ipatikane,” alisema Mhe. Ndejembi.
Katika kusimamia suala hilo, Waziri Ndejembi amemwagiza Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Tanga kukabidhi eneo hilo kwa mmiliki wake halali.
Aidha, Waziri Ndejembi amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita haitaki kuona mtu yeyote anaonewa au haki yake kupotea.
“Tumejipanga kuhakikisha haki inapatikana kwa kila mmoja, bila kujali nafasi yake katika jamii. Haki ni msingi wa maendeleo yetu,” aliongeza.
Hatua hii imepokewa kwa shukrani kubwa na Bw. Risasi, ambaye amepongeza jitihada za Waziri na Serikali kwa kusimamia haki za wanyonge.