DUWASA YAANZA KUREJESHA MIUNDOMBINU YA MAJI ILIYOSOMBWA NA MAFURIKO
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) leo Disemba 07,2024 imeanza kazi ya dharura ya urejeshaji wa miundombinu ya maji iliyosombwa na mafuriko kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Disemba 06,2024 katika Jiji la Dodoma na kuathiri miundombinu ya maji.
Timu maalum ya wataalamu na mafundi wa DUWASA imeingia uwandani katika maeneo mbalimbali yaliyopata athari hiyo kuhakikisha matengenezo yanakamilika ndani ya siku tatu kuanzia leo Disemba 07,2024 huku huduma ikirejeshwa maeneo ambayo matengenezo yanakamilika.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Meneja wa Kanda ya Nzuguni, Kelvin Swai amewahakikishia wananchi katika maeneo yote yaliyoathirika kwamba huduma itarejea kwa muda uliyopangwa kwa kuwa kilichotokea ni hali ya dharura.
Kelvin amesema kutokana na uharibifu wa miundombinu uliyotokea kutakuwa na ukosefu wa maji katika baadhi ya maeneo baada ya mabomba makubwa ya maji kusombwa na mafuriko Desemba 06, 2024.
Kelvin ameyataja maeneo yatakayoathirika ni Ihumwa SGR, SGR madukani, Njedengwa yote, Watumishi Housing, Iyumbu Shule ya mfano, Iyumbu kwa Anord, Nyumba 300 karibu na SGR, Mwangaza ya juu na Field Force Nyumba 300.
Maeneo mengine yatakayoathirika ni Martin Luther, Ilazo Zahanati, Ilazo Extension yote, Swaswa kidongo chekundu, Meriwa, Ipagala, Ipagala kanisa la Roma na Ilazo Daraja dogo pamoja na Mkonze Chinyika yote, Mkonze Zahanati, Michese yote, Michese Zahanati na Miganga South.
Aidha amewataka wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua za masika, kulinda miundombinu ya maji na kutoa taarifa pale wanapoona kuna athari imetokea katika maeneo yao.