MBIBO APONGEZA MWENENDO UKUSANYAJI MADUHULI TANGA
Mkoa wa Kimadini Tanga umepongezwa kwa mwenendo mzuri wa ukusanyaji Maduhuli ya Serikali yanayotokana na shughuli za Madini ambapo hadi kufikia Novemba 30, 2024 ulikusanya jumla ya shilingi bilioni 3.8 sawa na asilimia 120.9 ya lengo la miezi mitano ya Julai – Novemba, 2024. Katika mwaka wa Fedha 2024/25, Ofisi ya Madini Tanga imepangiwa kukusanya shilingi bilioni 8.
Hayo yalibainishwa Desemba 5, 2024, wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo alipotembelea ofisi hiyo kwa lengo la kukagua na kujionea shughuli za madini mkoani humo. Mbibo aliitembelea ofisi hiyo baada ya kushiriki na kufungua Mkutano wa Mwaka wa Wajiolojia nchini unaofanyika jijini Tanga.
Akizungumza katika kikao hicho, Mbibo aliwapongeza watumishi wa ofisi hiyo kwa kufikia malengo hayo na kusisisitiza kuendelea kufanya kazi kwa nidhamu, weledi na kuhakikisha wanatekeleza vision 2030, madini ni maisha na utajiri kwa manufaa ya taifa.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tanga Mhandisi Laurent Bujashi alisema miradi inayochangia kiasi kikubwa cha maduhuli ya Serikali mkoa wa Tanga kutokana na uzalishaji wa madini ni pamoja na kiwanda cha Tanga Cement Co. Ltd, Maweni Limestone Ltd, Godmwanga Gems Limited, Neelkanth Lime Limited, Ibrahimu Kuwasa & Ptns na Godfrey Stephen Bitesigirwe.
‘’ Mkoa wa Tanga umejaliwa kuwa na aina mbalimbali za madini yakiwemo madini ya metali, madini ya viwandani, madini ya vito na madini ujenzi,’’ alisema Mhandisi Bujashi.
Akizungumzia biashara ya madini kupitia masoko ya madini mkoani humo, alisema mkoa huo una jumla ya masoko mawili (2) yanayojumuisha soko la madini ya vito lililopo Wilaya ya Mkinga na Soko la madini ya dhahabu lililopo Wilaya ya Handeni.
‘’Pia tuna vituo viwili vya ununuzi wa madini; kituo cha ununuzi wa madini ya dhahabu Kikunde, Wilaya ya Kilindi na kituo cha ununuzi wa madini ya vito Kalalani, Wilaya ya Korogwe,’’alisema Bujashi.
Akielelezea mwenendo wa biashara ya madini kupitia masoko mhandisi Bujashi alisema katika kipindi cha Julai hadi Novemba 2024, masoko ya madini Mkoa wa Tanga yamewezesha mauzo ya madini ya vito kilogramu 31.64 yenye thamani ya milioni 132.7 na dhahabu kilogramu 24.09 yenye thamani ya bilioni 5.2 .
Kwa upande wa mikakati ya kuongeza ukusanyaji wa maduhuli, alisema ofisi hiyo imejiwekea mkakati kadhaa ikiwemo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo yenye uzalishaji na kusimamia masoko na vituo vya ununuzi wa madini, kuongeza vituo vya ukaguzi wa madini ujenzi na viwandani katika Wilaya za Korogwe, Lushoto na Pangani. Aliitaja mikakati mingine kuwa ni pamoja na ofisi kuendelea kutoa elimu kuhusu Sheria ya Madini Sura ya 123 na Kanuni zake kwa wachimbaji wadogo, Viongozi wa Serikali za Mitaa na Vijiji.