TCAA YATOA ELIMU YA USAFIRI WA ANGA NA FURSA ZILIZOPO KWA WANAFUNZI WA SEKONDARI YA MAKONGO
Katika kuelekea Maadhimisho ya Wiki ya Usafiri wa Anga Duniani, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa kushirikiana na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma ya Usafiri wa Anga (TCAA-CCC) imetembelea Shule ya Sekondari ya Makongo iliyoko Wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, Desemba 4, 2024.
Hii ikiwa ni muendelezo wa utoaji elimu kwa shule mbalimbali katika kuelekea kilele cha maadhimisho hayo.
Maafisa wa Mamlaka wametoa wito kwa wanafunzi kuweka juhudi katika masomo yao ili kuweza kuzikimbilia fursa zilizopo katika sekta ya usafiri wa anga nchini, hususani nafasi za kitaalamu kama Urubani, Uhandisi wa Ndege na Uongozaji Ndege ambazo zina uhaba mkubwa.
Akizungumza na wanafunzi hao, Afisa Mkuu Udhibiti Uchumi na Biashara wa TCAA , Bi Euphrasia Bille, alisema Mamlaka ina mfuko wa mafunzo unaotoa udhamini wa mafunzo ya Urubani na Uhandisi Ndege hivyo wenye nia ya kufanya kazi katika sekta ya Anga waongeze bidii katika masomo ili kuzinyakua fursa hizo za mafunzo hapo badae.
Kwa upande wake Bw. Benjamin Mayala Afisa Utawala wa TCAA, amefafanua kuwa, kutokana na upungufu mkubwa uliopo wa wataalam wazawa katika sekta ya usafiri wa anga, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania ilianzisha Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) kilochopo jijini Dar es Salaam ili kuweza kuzalisha watalaam wataosaidia kukabiliana na upungufu huo wa wataalam nchini.
Aidha, Bw. Mayala amewahimiza wanafunzi hao kusoma kwa bidii kwani ndio njia pekee ya kuwawezesha kujiunga na chuo hicho ili kuweza kupata utaalam wa kada mbalimbali ikiwemo uongozaji ndege, fundi sanifu, huduma za ndani ya ndege na uhandisi.
Nae Afisa Mwandamizi Elimu na Uchechemuzi kutoka Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Anga (TCAA-CCC), Bi. Debora Mligo alitoa elimu kuhusiana na haki za mtumiaji ikiwemo kupata taarifa sahihi pamoja na elimu, haki ya kupata usafiri ulio salama,haki ya kusikilizwa na kupatiwa fidia pale ambapo amepata madhara au kero kutoka kwa mtoa huduma.