DKT. TULIA ASHIRIKI IBADA MADHABAHU YA SAUTI YA UPONYAJI NA REHEMA ISYESYE JIJINI MBEYA
Rais wa Mabunge Duniani Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson ameshiriki ibada katika Madhabahu ya Sauti ya Rehema Kata ya Isyesye huduma inayoongozwa na Mchungaji Patrick Mwalusamba ambapo amewahimiza Waumini kuendelea kuombea amani nchini huku akiwasisitiza kushiki uchaguzi utakaofanyika novemba 27 mwaka huu.
Dkt Tulia Ackson amesema Waumini wanawajibu wa kwenda kusikiliza kampeni za uchaguzi ili wapate viongozi watakaowaletea maendeleo katika mitaa yao.
Aidha ameipongeza huduma hiyo kwa namna inavyozidi kukua siku hadi siku.
Dkt Tulia Ackson amesema Waumini wasiposhiriki kupiga kura wasiwe na sababu za kuwalaumu viongozi watakaochaguliwa kwa kuwa wao wameshindwa kuitumia fursa hiyo.
Amehitimisha kwa kuwashukuru Waumini kwa kumuombea Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na viongozi wote akiwemo yeye ndiyo maana amani inaendelea kuwepo nchini.
Awali Mchungaji Patrick Mwalusamba amempongeza Dkt Tulia Ackson kwa kufika ibadani licha ya majukumu mazito ya Jimbo,Taifa na Dunia.
Mwalusamba amesema uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu uwe huru na haki Ili nchi ipate viongozi watakaodumisha amani na kuwaletea maendeleo wananchi.
Mwalusamba amewahimiza Waumini wasikose kushiriki kupiga kura kwani hata biblia inasisitiza masuala ya uchaguzi.
Asifiwe Mwabukusi ameshukuru ujio wa Dkt Tulia Ackson kwenye ibada ilhali Getrude Chengula aliahidi kwenda kuwasikiliza wagombea na kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi.
Naye Victor Baraka muumini wa huduma hiyo amesema binafsi ujio wa Dkt Tulia Ackson umempa faraja kwani ni viongozi wachache wenye moyo kama wake na amehimiza wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa bila kujali itikadi zao.
Watanzania wanatarajia kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa novemba 27,2024 utakaowaweka madarakani viongozi wa vitongoji, vijiji na Mitaa uongozi utakaodumu kwa kipindi cha miaka mitano.