WANANACHI MOROGORO WAIPONGEZA EWURA KWA KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO YAO
Wadau mbalimbali wa mkoa wa Morogoro wametoa maoni, ushauri na kuwasilisha malalamiko yao kuhusu huduma zinazodhibitiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) katika mkutano wa wadau ulioandaliwa na EWURA Kanda ya Kati.
Mkutano huo uliofunguliwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa, ulilenga kupokea maoni na kutathimi hali ya utoaji huduma zinazodhibitiwa na EWURA mkoani hapo ambapo aliwataka wadau hao kutoa maoni na malalamiko bila woga, ili kuisaidia EWURA kuendelea kuboresha huduma za nishati na maji.
“Tuisaidie EWURA kuwasimamia watoa huduma, tutoe maoni yetu kwa ufasaha, uwazi na bila woga, ili huduma hizi za nishati na maji ziboreshwe kwa ustawi wetu”, alieleza.
Dkt. Musa pia, ameisihi EWURA, kuisimamia kwa karibu Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Morogoro (MORUWASA), ili watoe huduma bora na fanisi kwani kumekuwapo malalamiko juu ya kukosekana kwa huduma ya maji mara kwa mara.
Wadau walioshiriki mkutano huo ni kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Manispaa, wamachinga, walimu, wajasiriamali, wafanya biashara, viongozi wa dini, madereva bajaji na bodaboda. Wengine ni watu wenye ulemavu, watoto, wazee, jukwaa la wanawake, EWURA CCC, MORUWASA na TANESCO.
Meneja wa EWURA Kanda ya Kati, Mha. Hawa Lweno, alisisitiza kuwa, malalamiko na maoni yaliyopokelewa yatafanyiwa kazi kwa wakati ili watumia huduma za nishati na maji mkoani hapo wafurahie huduma bora.