MHANDISI SAMAMBA AWASISITIZA MAAFISA MADINI KUSIMAMIA USALAMA WA MIGODI HASA KATIKA MSIMU HUU WA MVUA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Ismail Samamba amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuweka nguvu kwenye usimamizi wa usalama na mazingira kwenye migodi ya madini hasa katika msimu huu wa mvua ili kuepuka ajali zinazoweza kutokea na kusababisha vifo.
Mhandisi Samamba ametoa agizo hilo leo Novemba 21, 2024 jijini Dar es Salaam kwenye kikao chake na menejimenti ya Tume ya Madini ikijumuisha Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa.
“Ninawataka kufanya ukaguzi mkubwa kwenye migodi yote ya madini nchini hasa katika kipindi hiki cha mvua na kusitisha shughuli za uchimbaji wa madini katika maeneo hatarishi ili kuepuka ajali zinazoweza kutokea,’’ amesisitiza Mhandisi Samamba.
Katika hatua nyingine,amewapongeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kwa mwenendo bora wa ukusanyaji wa maduhuli na kuwataka kuendelea kuwa wabunifu ikiwa ni pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.
“ Katika kipindi cha kwanza cha mwaka wa fedha 2024/2025 mwenendo wa makusanyo ya maduhuli ambapo mpaka sasa wastani wa kiasi cha shilingi bilioni 395 zimeshakusanywa, nawapongeza kwa kazi nzuri sana na kuwataka kuongeza ubunifu kwenye ukusanyaji wa maduhuli pamoja na kuwepo kwa changamoto ya kushuka kwa bei ya dhahabu kwenye soko la dunia na kipindi cha mvua ambacho kinatarajiwa kuanza hivi karibuni,’’ amesisitiza Mhandisi Samamba.
Katika hatua nyingine amewataka maafisa hao kutoa elimu kwa wadau wa madini kuhusu fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini katika mikoa yao kupitia warsha, maonesho na makongamano mbalimbali.
Aidha, amewataka kuendelea kusimamia kwa karibu watumishi waliopo chini yao na kusisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutatua changamoto ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kutosha na uboreshaji wa maslahi ya watumishi.