ATUPWA JELA MAISHA KWA KUMBAKA MTOTO WA MIAKA 8
Mahakama ya Wilaya ya Kwimba Mkoa wa Mwanza imemhukumu kifungo cha maisha jela Samwel Anthony (34) mkazi wa kijiji cha Shilima kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka nane.
Hukumu hiyo imetolewa Novemba 20, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu Ndeko Dastan Ndeko ambaye ndio Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo baada ya kusikiliza mashahidi watano wa Jamhuri akiwemo Mhanga na Mahakama imejiridhisha pasi na kuacha shaka kwamba mtuhumiwa ametenda kosa hilo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa na mwendesha mashtaka wa Serikali Juma Kiparo, mtuhumiwa alitenda kosa hilo Agosti 16, 2024 huko maeneo ya kijiji cha Shilima, Wilaya ya Kwimba Mkoa wa Mwanza.
Mhanga ambaye jina lake linahifadhiwa kwasababu za kisheria, alifanyiwa kitendo hicho wakati ameagizwa na mama yake dukani na wakati anarudi ndipo mtumiwa alimvuta nyuma ya nyumba ya baba wa mhanga kisha kumfanyia ukatili huo.
Mshtakiwa alifikishwa mahakamani tarehe 23.08.2024 na kusomewa shtaka la kubaka kinyume na kifungu cha 130 (1)(2)(e) na 131 (3) vya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 ya Sheria marejeo ya mwaka 2022.