WAZIRI MKUU AFUNGUA MKUTANO WA KIMATAIFA SEKTA YA MADINI

0

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ametoa Maagizo kwa Wizara ya Madini kuhakikisha inasimamia vyama vya wachimbaji wadogo wa madini ili wanazingatia sera na sheria zilizopo za uchimbaji jambo ambalo litasaidia na kuchangia maendeleo ya kiuchumi.

Akizungumza leo Novemba 19, 2024, jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini, Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa amesema kuwa sekta ya madini inatakiwa kuendelea kasi katika utendaji wa kazi.

Mhe. Majaliwa amesema kuwa serikali imejipanga kuboresha zaidi mazingira ya wachimbaji wadogo ili kuhakikisha hadi ifikapo mwaka 2030 wachimbaji wadogo wanakuwa wachimbaji wa kati na kuongeza mchango katika uchumi wa Taifa.

“Nawaelekeze Wizara ya Madini kuendelee kusimamia vyama vya wachimbaji madini, hatua hii itasaidia kukuza na kuimarisha soko la madini na kuvutia wawekezaji” amesema Mhe. Majaliwa.

Mhe. Majaliwa amewahamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta ya madini, huku akisisitiza Tanzania imejipanga kimkakati kupitia maeneo yanayofaa kwa uwekezaji.

Amebainisha kuwa serikali imefanya mapitio ya sera na inaendelea na mchakato wa kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo kwa kutumia maeneo yaliyorejeshwa.

Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya madini yamechochewa na uongozi bora wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Mavunde amesema kuwa serikali imeongeza bajeti ya sekta katika sekta ya Madini kutoka shilingi bilioni 89 hadi bilioni 231 ili kuimarisha zaidi utendaji katika sekta hiyo.

Waziri Mavunde amesema kuwa kuwa sera mpya ya kuongeza thamani ya madini inalenga kutoa ajira kwa vijana wengi na kuongeza mchango wa sekta katika pato la taifa.

Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini umebeba kauli mbiu isemayo “Uongezaji Thamani ya Madini kwa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii.”, Mkutano huu umeleta fursa ya kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa sekta ya madini, wawekezaji na serikali kwa kuendeleza rasilimali za madini kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *