WAZIRI MKUU ASHUHUDIA HALI YA UOKOAJI KARIAKOO

0

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameviagiza vyombo vyote vya usalama vihakikishe watu wote waliokwama ndani ya jengo lililoporomoka katika kata ya Kariakoo jijini Dar es Salaam wanaokolewa huku mali zao zikilindwa.

Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Novemba 16, 2024) baada ya kushuhudia juhudi za uokoaji zinavyoendelea baada ya jengo ghorofa nne kuporomoka katika eneo la Karikoo.

Akizungumza baada ya kukagua juhudi za uokoaji katika eneo hilo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Majaliwa amesema hadi sasa watu 40 mejeruhiwa ambapo 33 wameruhusiwa na saba wanaendelea na matibabuna mmoja amefariki.

“Ndugu zangu nimekuja kuona hali ya uokoaji inavyoendelea na kutoa pole kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pia ninawashukuru wananchi kwa ushiriki wenu tangu tukio hili lilivyotokea”

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia Watanzania kuwa kazi kubwa ya uokoaji inaendelea na vyombo vyote vya ulinzi na uokoaji vipo katika eneo hilo, hivyo amewataka waendelee kuwa na subra.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amemuelekeza Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi kusimamia uchuguzi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo. “Watalaam mnaohusika na masuala ya ujenzi fanyeni ukaguzi wa ujenzi wa majengo unaoendelea”

Waziri Mkuu amesisitiza kwamba kazi ya uokoaji itaendelea hadi kuhakikisha anatolewa hadi mtu wa mwisho. “Nikiwa hapa nimeona mtu mmoja ametoka na amesema wenzake wapo chini,”

Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewatembelea majeruhi wa ajali hiyo waliolazwa kwenye hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *