DKT. MPANGO AFUNGUA MKUTANO WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA COP 29 – AZERBAIJAN
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema dhamira imara ya kisiasa katika ngazi zote za kitaifa na kikanda ni muhimu katika kuondoa matumizi ya nishati chafu ya kupikia ili kuendeleza sera, mikakati, mipango na malengo ya kufikia matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa pembezoni wa nishati safi ya kupikia uliyoandaliwa na Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika (AU) pamoja na Tume ya Nishati Afrika (AFREC) uliyofanyika wakati wa Mkutano wa 29 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaofanyika katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan.
Amesema usambazaji wa nishati safi ya kupikia ni nguzo muhimu katika ustawi wa jamii hivyo ni muhimu kuongeza jitihada za kuwezesha upatikanaji wake kwa gharama nafuu ili kuikomboa jamii hususani wanawake. Ameongeza kwamba upatikanaji wa nishati safi ya kupikia utachochea usawa wa kijinsia kwa kuwa utawawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika elimu, kuepushwa na athari za kiafya zinazosababishwa na nishati chafu pamoja na kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kiuongozi.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa Viongozi wa Afrika na jumuiya ya kimataifa kuongeza ushirikiano ili kuwa na nguvu ya pamoja katika kuendelea kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia. Pia, amesisitiza mchakato wa utekelezaji wa nishati safi ni muhimu kuzingatia mazingira ya nchi husika ikiwemo rasilimali zilizopo, changamoto, mahitaji ya jamii husika na teknolojia za asili. Kadhalika, mchakato huo kufanyika kwa hatua kwa kukizingatia idadi kubwa ya Waafrika wanategemea nishati ya kuni na mkaa.
Makamu wa Rais amesisitiza Viongozi wa Afrika kutoa kipaumbele cha pekee katika suala hilo kwa ushirikiano na wabia kutoka taasisi za kimataifa na sekta binafsi. Amesema kutokana na Afrika kuwa na idadi kubwa ya vijana ni muhimu kutumia ubunifu wa vijana hao katika kuendeleza teknolojia sahihi ya nishati safi ya kupikia. Ameongeza kwambani muhimu kutoa msisitizo katika vyuo vya ufundi na ujuzi katika masuala ya teknolojia za nishati safi ya kupikia ili kuongeza rasilimali watu muhimu katika uvumbuzi wa teknolojia za kupika kisasa pamoja na matengenezo ya vifaa vinavyotumika kupika kisasa.
Kadhalika Makamu wa Rais amesisitiza matumizi ya teknolojia ya kidigitali ikiwemo utaratibu wa malipo ya kabla (prepaid system) ili kuhakikisha uwazi na haki katika matumizi ya nishati safi. Aidha, amesema katika uunganishaji wa huduma hiyo ni vyema kuwe na chaguo la malipo kidogokidogo ili kuwezesha watu wengi wa kipato cha chini hususani vijijini kufikiwa na huduma hiyo.
Makamu wa Rais amesema kuzinduliwa kwa programu ya nishati safi ya kupikia ya kuwasaidia wanawake barani Afrika katika mkutano wa COP28 Dubai pamoja na Kuzinduliwa kwa Mkakati wa Tanzania wa Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia 2024 – 2034 ni jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuonesha njia na kuhimiza viongozi wa Afrika kulipa kipaumbele suala hilo.