BUNGE BONANZA KUANZA KUTIMUA VUMBI JANUARI 2025
Mwenyekiti wa Bunge Bonanza, Mhe. Festo Sanga, amezindua maandalizi ya Bunge Bonanza la kwanza kwa Mwaka wa 2025, huku mgeni wa rasmi anatarajiwa kuwa Spika wa Bunge la Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge ya Duniani (IPU) Mhe. Dkt. Tulia Ackson.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 12, 2024 katika Ofisi Ndogo za Bunge, Jijini Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bunge Bonanza Mhe. Festo Sanga, amesema kuwa bonanza hilo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya @azaniabankplc na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo limebeba kauli isemayo UTANI WETU, UMOJA”.
Mhe. Sanga amesema kuwa katika bonanza hilo kutakuwa na mgeni wa heshima ambaye ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia, huku akieleza bonanza litahusisha michezo mbalimbali kati ya Wabunge na Watumishi wanaoshabikia timu za Simba SC na Yanga Sc wakiwa na lengo la kuhamasisha jamii kushiriki michezo ili kujenga afya, kutoa burudani pamoja na kudumisha umoja na mshikamano.
Mhe. Sanga amesema kuwa miongoni mwa michezo itakayokuwepo ni pamoja na Mpira wa miguu, Kikapu, Pete, Meza, Kuvuta kamba, Pool Table, Riadha, Kutembea mwendo wa haraka, Kucheza bao, Draft, Kuruka tufe, Karata, Vishale, Kukimbia na Gunia, Kufukuza kuku, Kujaza maji katika chupa, Kushindana kunywa soda, Kula chakula kwa haraka.