ZINGATIENI WELEDI, MAADILI, SHERIA NA MIONGOZO UANDISHI WA HABARI ZA UCHAGUZI
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo Bi. Zamaradi Kawawa amewataka Waandishi wa Habari nchini kuendelea kutumia weledi, maadili, sheria na miongozo ya uchaguzi katika kuandika Habari zinazohusu uchaguzi wa serikali za mitaa huku wakitoa haki na usawa kwa vyama vyote vya siasa nchini.
Bi. Kawawa ametoa rai hiyo wakati akifungua semina ya siku mbili ya kuwajengea uwezo waandishi wa Habari, kuandika Habari za uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka 2024 iliyoandaliwa na mtandao wa mashirika yanayotoa msaada wa kisheria Tanzania TANLAP Jijini Dodoma.
“Tunatarajia kuwa vyombo vya habari vitaripoti mchakato mzima kuelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa ikiwemo Kampeni na matokeo ya uchaguzi kwa kuzingatia weledi, maadili, sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya uandishi wa Habari, na uchaguzi katika nchi yetu,”amesema.
Naye Meneja wa huduma za utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mha. Endrew Kisaka amewasisitiza waandishi kutopendelea chama chochote ikiwa ni pamoja na kuzingatia usawa wakati wa kuripoti habari zao.
“Mkiwa kwenye vipindi msipendelee chama chochote na mnapoandaa midahalo hakikisheni wagombea wanasema sera zao na siyo kumsema mtu au kusema chama kingine,”amesema Mha. Kisaka.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini OR – TAMISEMI Bi. Nteghenjwa Hoseah akiwasilisha kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 amesema uchaguzi huo unaongozwa na kanuni nne kwa mujibu wa tangazo la serikali na. 571,573, 574 na 572 la mwaka 2024.