TANZANIA YAN’GARA MIRADI YA KINYWE

0

Ripoti ya Benki ya Dunia na Takwimu za Taasisi ya Jiolojia ya Marekani kuhusu makisio ya utajiri wa mashapo ya Madini ya Kinywe ifikapo mwaka 2050 imeitaja nchi ya Tanzania kushika nafasi ya Sita (6) Duniani na nafasi ya Tatu (3) Afrika huku Msumbiji ikishika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Madagasca kwa upande wa nchi za Afrika.

Hayo yamebainishwa Novemba 7, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance wakati akimwakilisha Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde katika mjadala wa Mawaziri ‘Ministerial session’ uliofanyika katika Kilele cha Mkutano wa Madini Muhimu Afrika uliofanyika Cape Town, Afrika Kusini na kuongeza kwamba, Tanzania imebarikiwa kuwa na aina nyingi za madini muhimu yanayohitajika kwa ajili ya uzalishaji wa nishati na teknolojia za kisasa.

Alisema Tanzania imejipanga katika ugunduzi wa madini ya kinywe na madini mengine ya nishati safi kama nikeli, Cobalt, lithium, rare earth elements na nobium kwa kuwa na taarifa za kutosha za kijilojia.

‘’Tanzania imeanza kutekeleza Madini Vision2030 yenye lengo la kupunguza uwezekano wa wawekezaji kupata hasara kwa kufanya tafiti maeneo ambayo hayana taarifa za kijilojia ‘derisking the sector’. Lengo la mkakati huo ni kufanya utafutaji wa madini kwa njia ya ndege (High Resolution Airbone Survey) kutoka asilimia 16 ya sasa na kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030’’

Dkt. Mwasse alieleza kuwa ni muhimu sasa kwa nchi za Afrika kuwa na ushirikiano wa kuongeza thamani madini muhimu kwa kuweka viwanda katika nchi ambayo itakuwa inafaa kwa nchi nyingine za afrika. “Ni wakati mwafaka wa nchi za Afrika kufanya uchambuzi wa faida na hasara ‘cost benefit analysis” kuona sehemu sahihi ya kuweka mitambo ya kusafisha na kuongeza thamani madini muhimu” aliongeza “mfano kiwanda kitakachojengwa cha Kabanga Nickel multi-metal smelter cha kahama kitawezesha nchi jirani kama Burundi na Congo kusafisha madini yao pale ili wananchi wawe na ustawi kutokana na rasilimali za nchi yao na ilikufanikiwa katika jambo hili ni muhimu kuwa na ushirikiano baina ya nchi za Afrika,’’ alisisitiza Mwasse.

Aliongeza kwamba, Tanzania inaliimarisha Shirika lake la STAMICO ili kuvutia uwekezaji kwa kuwa na leseni zake ambazo inazifanyia utafiti kupunguza muda ambao mwekezaji anageutumia kuanza kufanya utafiti na uwezekano wa kupata hasara kwa kutokuwa na uhakika wa uwepo wa mashapo.

“Ni wakati mwafaka kwa nchi za Afrika kuimarisha Mashirika yao ya Madini yanayomilikiwa na nchi zao kuendeleza madini Muhimu na kuongeza manufaa ya nchi,’’ alisema Dkt. Mwasse.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *