SERIKALI KUANZISHA PROGRAMU MPYA YA TAIFA YA LISHE BAADA YA KUFUTWA TFNC

0

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, ameeleza kuwa Serikali imeanza mchakato wa kuanzisha Programu ya Taifa ya Lishe kufuatia uamuzi wa kufutwa kwa Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC).

Dkt. Mollel ameyasema hayo leo Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Dkt. Alice Karungi Kaijage mbunge wa Viti Maalum ambapo alitaka kujua haja ya Serikali kuhuisha Taasisi ya Lishe badala ya kuifuta kabisa

“Wizara ya Afya inatarajia kuanzisha Programu ya Taifa ya Lishe pamoja na kuanzisha Kitengo cha utafiti wa lishe katika Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR). Hivyo, yale majukumu yaliyokuwa yanatekelezwa na TFNC yatafanyika kwa upana wake na Programu ya Taifa ya Lishe,” amesema Dkt. Mollel

Aidha Dkt. Mollel amesema tamko la kufutwa kwa TFNC lilitolewa na Msajili wa Hazina mnamo Desemba 15, 2023, na kwamba majukumu yaliyokuwa yakitekelezwa na taasisi hiyo sasa yatahamishiwa kwenye Programu ya Taifa ya Lishe pamoja na kitengo kipya cha utafiti wa lishe ndani ya Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

Pia, Naibu Waziri ameongeza kuwa hatua za awali za kuanzisha programu hiyo tayari zimeanza, hatua inayolenga kuboresha masuala ya lishe na utafiti wa kisayansi nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *