DENI LA SERIKALI LA ONGEZEKA HADI TRIL. 96

0

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema hadi kufikia mwezi June mwaka huu 2024, deni la Serikali liliongezeka na kuwa Tsh. bilioni 96,884.18 (Tsh. trilioni 96.8) ambapo Kati ya kiasi hicho, deni la ndani lilikuwa shilingi bilioni 31,951.24 na deni la nje lilikuwa shilingi bilioni 64,932.94.

Akiongea leo November 01,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/2026, Prof. Mkumbo amesema fedha zilizosababisha deni hilo zilielekezwa katika kugharamia miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme na maji

“2023/24 kampuni za Fitch Ratings na Moody’s Investors Service zilifanya mapitio ya tathmini ya Nchi kukopesheka katika masoko ya mitaji ya kimataifa na kuchapisha matokeo ya daraja B1 na B+ mtawalia, matokeo mazuri ya tathmini hizo yalitokana na ukuaji mzuri wa uchumi unaoweza kuhimili mitikisiko ya kiuchumi, utekelezaji wa mageuzi ya kimuundo yanayoboresha mazingira ya biashara, ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa fedha za umma, matokeo hayo yatawezesha kupungua kwa gharama za mikopo (riba za mikopo) kutokana na kuongezeka kwa imani kwa Wakopeshaji na hivyo kuwezesha ugharamiaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, kuongezeka kwa uwekezaji kutoka nje ya Nchi ambao utasaidia kukuza uchumi”

Itakumbukwa wakati akitoa hotuba ya hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2023, Bungeni Jijini Dodoma June 13,2024, Waziri Mkumbo alisema hadi kufikia March 2024, deni la Serikali lilikuwa shilingi bilioni 91,708.3 (Tsh. trilioni 91.7) ikilinganishwa na shilingi bilioni 77,010.4 (Tsh. trilioni 77.) katika kipindi kama hicho mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 19.1.

Kwa upande wake CAG Charles Kichere, wakati akiwasilisha ripoti kuu kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa Rais Samia Ikulu Dodoma March 28,2024 alisema hadi kufikia June 30,2023 deni la Serikali lilikuwa Tsh. trilioni 82.25 sawa na ongezeko la 15% kutoka Tsh.trilioni 71.31 kwa mwaka 2021/2022.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *