WABUNIFU MAJENGO NA WAKADIRIAJI MAJENZI ZINGATIENI SHERIA – BALOZI AMOUR
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi, Mhandisi Aisha Amour amewataka Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni za utendaji kazi ili kupata majengo bora, salama yasiyoathiri mazingira na yanayoendana na thamani halisi ya fedha.
Akizungumza Oktoba 30, 2024 jijini Dar es Salaam, wakati akifunga Mkutano wa Tano wa mwaka wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Balozi Amour amesisitiza kuzingatia miiko ya taaluma hiyo na kufanya juhudi za makusudi za kujifunza uendelezaji wa majenzi nchini kwa kutumia mbinu za kiteknolojia za kisasa ili kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia.
“Niipongeze Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) kwa kuendelea kusimamia wataalam hawa na kuendelea kutoa ushauri wa kitaalam kwa miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini ili kusaidia kupunguza malalamiko ya weledi na ujuzi wa utekezaji wa miradi nchini”, amesema Balozi Amour.
Amesisitiza wataalamu hao kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha mkakati wa kuinua wazawa kupitia fani hiyo unafanikiwa kutokana na kupata fursa za kushiriki katika utekelezaji wa miradi mikubwa nchini.
Aidha, Balozi Amour ametoa rai kwa Kampuni za ndani kushiriki katika michakato yote ya zabuni ya miradi mikubwa ili hatimaye kujijengea uwezo wa kitaaluma na kupunguza utegemezi wa wataalam kutoka nchi za nje kwa kazi za ujenzi na matengenezo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) Dkt, Ludigija Bulamile amesema kuwa Bodi imesajili wahitimu 873 waliomaliza masomo yao kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali nchini lengo ni kuhakikisha wahitimu wote wanasajiliwa ndani ya kipindi cha miaka miwili baada ya kuhitimu masomo yao.
Ameipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kuiwezesha Bodi hiyo kutembelea na kukagua miradi mingi ili kujionea utekelezaji wake katika maeneo mbalimbali nchini.
Mkutano huo wa Siku mbili ambao umemalizika leo umeongozwa na mada kuu isemayo “Mabadiliko ya Mbinu na Teknolojia katika Sekta ya Ujenzi Tanzania” na umeshirikisha wataalamu wa kada ya Ubunifu Majengo na Ukadiriaji Majenzi kutoka mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi.