RAIS SAMIA APAMBANIA MFUKO WA MAJI WA TAIFA
Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) unafanikisha ujenzi wa miradi ya maji katika maeneo yenye uhitaji mkubwa hapa nchini.
NWF inalo jukumu la msingi la kutafuta fedha za utekelezaji wa miradi ya maji, mjini na vijijini ambapo Serikali ya awamu ya sita inahakikisha jambo hilo linafanikiwa kwa wananchi kufikiwa na huduma ya majisafi.
Mtendaji Mkuu wa NWF Bw. Haji Nandule amesema hayo jijini Dar es salaam katika kikao na vyombo vya habari na kusisitiza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanikisha upatikanaji na matumizi ya fedha ambapo asilimia 60 ya fedha hizo zinapelekwa katika kufanikisha miradi ya maji vijijini kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Amesema NWF imefungua Dirisha la Mkopo Wenye Masharti Nafuu mahsusi katika kutekeleza miradi ya maji kwa mamlaka za maji hapa nchini na tangu mwezi Julai 2024 kiasi cha shilingi bilioni 5.3 kimetolewa kama mkopo kwa mamlaka za maji za Tanga UWASA, Bunda na Dar es salaam (DAWASA).
Mwenyekiti wa Bodi ya NWF Mhandisi Abdallah Mkufunzi amesema taratibu za kutoa mkopo hiyo zinapitiwa zaidi ili kuweza kuimarisha ujenzi wa miradi ya maji na uendelevu wake kwa faida ya wananchi.
Naye, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Bw. Prosper Buchafwe amesema Serikali inao mgawanyo wa majukumu na kila taasisi ya Wizara ya Maji inalo jukumu lake la msingi, NWF ikiwa na kazi ya kutafuta fedha, wakati mamlaka za maji zikiwa na jukumu la msingi la kutoa huduma maji kwa wananchi.