NHC WAFANYA UKARABATI MKUBWA NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU KONGWA

0

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limekamilisha ukarabati mkubwa wa nyumba za gharama nafuu wilayani Kongwa, mkoani Dodoma. Hatua hii imeongeza ubora wa makazi kwa wapangaji na kutoa fursa kwa wananchi wa kawaida kumiliki nyumba hizo kwa masharti nafuu.

Nyumba hizi zilizoboreshwa zimefungua milango kwa wananchi wenye kipato cha kawaida kupanga au hata kununua, huku NHC ikitoa utaratibu rafiki wa kumiliki makazi. Kupitia mikopo yenye masharti nafuu inayotolewa na taasisi mbalimbali za fedha, wakazi wa Kongwa sasa wanapata nafasi ya kumiliki nyumba hizo kwa gharama nafuu, na wanashauriwa kufika katika ofisi za NHC ili kupata maelezo zaidi kuhusu vigezo na taratibu za ununuzi.

Wananchi waliozungumza na wawakilishi wa NHC walieleza kuridhishwa kwao na ubora wa nyumba hizo na kutoa shukrani zao kwa Shirika kwa juhudi za kuwapatia makazi bora kwa bei nafuu. “Tunafurahia kuona Shirika la Nyumba la Taifa linajali na kuwekeza katika maeneo yetu kwa kutupa makazi bora. Hii ni hatua kubwa kwetu,” alisema mmoja wa wapangaji wa nyumba hizo.

NHC imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kushikamana na juhudi za Serikali za kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora na nafuu. Shirika limesisitiza dhamira yake ya kuimarisha huduma za makazi nchini kwa kuendeleza ukarabati wa nyumba nyingine katika maeneo mbalimbali nchini kote. Mradi huu umetoa mfano mzuri wa jinsi NHC inavyoboresha makazi na kuimarisha hali ya maisha ya wananchi.
Wiki iliyopita Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya NHC, Bi. Dorothy Mwanyika, pamoja na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Shirika walifanya ziara maalum kukagua maendeleo ya mradi huo ambao umekamilika kwa mafanikio na sasa una wapangaji wenye kuridhika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *