WAZIRI CHANA AWASILI MKOANI SINGIDA KUTATUA CHANGAMOTO YA TEMBO
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amewasili katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida leo Oktoba 28,2024 kwa ajili ya kupatia ufumbuzi changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo katika Wilaya hiyo.
Mhe. Chana amepokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mhe.Thomas Apson ambapo pamoja na mambo mengine amepokea taarifa kuhusu hali ya udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu Mkoani Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego akizungumza katika kikao cha awali ametoa maelezo kuhusu tukio la tembo lililotokea katika eneo la Kambi ya Mkaa Wilayani Ikungi Oktoba 26,2024 ambalo lilisababisha taharuki kwa wananchi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Alex Lobora, Kamishna Uhifadhi Msaidizi Mwandamizi na Mkuu wa Kanda ya Kati, Herman Nyanda pamoja na baadhi ya Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, TAWA na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Singida.