KAIMU MWENYEKITI BODI YA NHC APONGEZA MATENGENEZO YA NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU KONGWA
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bi. Dorothy Mwanyika, ameongoza ziara ya ukaguzi wa nyumba zilizofanyiwa matengenezo makubwa wilayani Kongwa, mkoani Dodoma. Ziara hiyo ilijumuisha pia baadhi ya wajumbe wa menejimenti ya Shirika, ambapo walipata fursa ya kujionea maendeleo ya mradi huo ambao umekamilika na nyumba hizo kwa sasa zina wapangaji.
Katika ziara hiyo, Bi. Mwanyika alionyesha kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa na NHC katika kuboresha nyumba hizo ambazo awali zilikuwa zimechakaa. Alieleza kuwa Shirika limejikita katika kuhakikisha kwamba nyumba zinazomilikiwa zinadumu na zinakidhi mahitaji ya jamii. “Tumejitahidi kuboresha nyumba hizi kwa kiwango cha juu ili kuhakikisha wapangaji wanaishi kwa amani na katika mazingira mazuri. Hii ni sehemu ya mkakati wetu wa kuboresha huduma zetu kwa wananchi,” alisema Bi. Mwanyika.
Nyumba hizo za gharama nafuu, ambazo zimetengenezwa kwa ubora wa hali ya juu, sasa zinahudumia wakazi wa Kongwa na kutoa fursa kwa wananchi walio na kipato cha kawaida kuweza kumudu kupanga na hata kumiliki nyumba hizo. Katika mchakato wa ununuzi, wananchi wanashauriwa kufika katika ofisi za NHC ili kupata maelezo zaidi kuhusu taratibu na vigezo vinavyohitajika.
Aidha, NHC imetangaza kuwa nyumba hizo sasa zinapatikana kwa ajili ya ununuzi kwa wananchi wanaotaka kumiliki makazi yao wenyewe. Shirika limeweka utaratibu rafiki kwa wananchi wenye nia ya kununua nyumba hizo, ikiwa ni pamoja na mikopo yenye masharti nafuu kupitia taasisi za fedha zilizopo. Hii ni fursa adhimu kwa wananchi wa Kongwa na maeneo jirani kuwekeza katika makazi yao ya kudumu kwa gharama nafuu.
Wananchi waliozungumza na ugeni huo walitoa shukrani zao kwa NHC kwa juhudi za kuboresha nyumba hizo na kuwapa fursa ya kumiliki nyumba kwa gharama nafuu. “Ni furaha kwetu kuona Shirika la Nyumba la Taifa linajali na kuwekeza katika maeneo yetu kwa kutupa makazi bora. Hii ni hatua kubwa kwetu,” alisema mmoja wa wapangaji wa nyumba hizo.