WAZIRI SILAA ATINGA IRAMBA KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO
- Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb.) leo Oktoba 23, 2024 ameendelea na ziara yake ya kutembelea, kukagua, na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo ametembelea miradi ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami, ujenzi wa Chuo cha Ufundi (VETA) Iramba, pamoja na mradi wa shule ya sekondari ya Lulumba.
Barabara ya Kiwango cha Lami
Waziri Silaa amekagua mradi wa barabara ya kiwango cha lami inayojengwa kuunganisha mikoa ya Singida, Simiyu na Arusha. Mradi huu, wenye thamani ya shilingi bilioni tisa, umefikia asilimia 65 ya utekelezaji.
Amesema Serikali inafanya kazi kubwa katika kutekeleza mradi huo, ambao unatarajiwa kuboresha huduma za usafiri. Pia, Waziri Silaa alionesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi, akisisitiza kwamba hakuna ubabaishaji.
Ujenzi wa Chuo cha Ufundi (VETA)
Mradi mwingine ni ujenzi wa Chuo cha Ufundi (VETA) wilaya ya Iramba mkoani Singida, ambao unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.4.
Shule ya Sekondari Lulumba
Waziri Silaa amekagua ujenzi wa madarasa mapya matano (5) pamoja na matundu 15 ya choo katika shule ya sekondari Lulumba, wenye thamani ya Tsh 134,000,000. Kati ya fedha hizo, Tsh 110,000,000 zimetumika katika ujenzi wa madarasa, na Tsh 24,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyoo.
Katika ziara hiyo, Waziri Silaa ameagiza Wizara yake kuhakikisha wanapatia shule hiyo huduma ya intaneti ya bure (Free Wi-Fi) pamoja na chumba chenye kompyuta kwa ajili ya masomo ya TEHAMA.
Bunifu za Wanafunzi
Waziri Silaa amejionea bunifu mbalimbali zilizofanywa na wanafunzi wa shule hiyo, ikiwemo kifaa cha kuchomelea mageti na mashine ya kufulia. Alipokea pia zawadi ya picha kutoka kwa mwanafunzi wa shule hiyo.
Mradi huu una lengo la kuongeza idadi ya wanafunzi pamoja na kutengeneza mazingira rafiki ya kujifunzia.
Ziara katika Ziwa Kitangiri
Waziri Silaa ametembelea ziwa Kitangiri lililopo kijiji cha Tulya, kata ya Tulya, tarafa ya Kisiriri na kuzungumza na wananchi wanaofanya shughuli za uvuvi katika eneo hilo.