RAIS RUTO KUTEUA NAIBU RAIS MPYA
Muda mfupi baada ya Bunge la Seneti kumvua madaraka Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua jana usiku, Spika wa Seneti, Amason Kingi, alichapisha katika gazeti rasmi la serikali uamuzi huo, hivyo kuthibitisha rasmi kuondolewa kwake katika wadhifa wa Naibu Rais wa Kenya.
Taarifa hiyo ya gazeti, yenye tarehe ya jana, Oktoba 17, 2024, ilitolewa mara baada ya Seneti kupitisha hoja ya kumwondoa ofisini Gachagua.
Katika tangazo hilo, Spika wa Bunge la Seneti ameorodhesha hoja tano kati ya 11 zilizosababisha uamuzi wa kumwondoa Gachagua ofisini.
Baada ya kuondolewa kwa Gachagua, Rais William Ruto anatarajiwa muda wowote kuanzia sasa kumteua Naibu Rais mpya na kuwasilisha jina hilo kwenye Bunge la Taifa kwa ajili ya idhini na ‘kumpiga msasa’.
Kuna taarifa kwamba Bunge la Kitaifa linajipanga kukutana leo na pengine ni kujadili jina litakalopendekezwa na Rais Ruto.
Wachunguzi wa mambo wanasema kwamba huenda mpango ni kumpata Naibu Rais mpya kabla ya Siku Kuu ya Mashujaa (zamani Kenyatta Day), itakayofanyika keshokutwa Jumapili, Oktoba 20.
Hata hivyo, inasemekana kwamba mawakili wa Gachagua wanajiandaa kutinga mahakamani muda wowote kupinga kuteuliwa kwa Naibu Rais mwingine na kuapishwa kwake na moja ya hoja zao ni kwamba mteja wao, Gachagua ambaye aliugua jana na kulazwa, hakupewa nafasi ya kujibu mashitaka dhidi yake mbele ya seneti kinyume na haki za msingi za mtu kusikilizwa kabla ya kuhukumiwa.
Jana, Bunge la Seneti lilikataa hoja za mawakili wa Gachagua la kutaka kuahirisha mchakato wa kuendelea na kusikiliza shauri la mteja wao wakisema hawawezi pia kuendelea kuwepo kwenye Seneti kwa sababu mteja wao hayupo ili kuwaelekeza cha kusema.
Mmoja wa mawakili wa Gachagua ameandika kwenye mtandao wa X (zamani Twitter) kwamba ‘Mapambano bado yanaendelea.’
Chanzo: Citizen Kenya na mitandao ya kijamii