JKCI KUSHIRIKIANA NA HOSPITALI ZA ARUSHA KUKUZA UTALII WA MATIBABU
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ya Jijini Dar Es salaam JKCI imeingia mashirikiano ya kitabibu kati yake na Hospitali mbili za Mkoa wa Arusha ambazo ni Hospitali ya Mkoa Mount Meru na Seliani Lutheran Medical ili kutoa huduma za matibabu bobezi na ya Kibingwa kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha na Kanda nzima ya Kaskazini.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amewaambia wanahabari kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia kwa Waziri wa TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa, akitaka Hospitali zote kuwa na huduma za Kibingwa ili kutoa urahisi wa wananchi kupata matibabu hayo katika maeneo ya karibu bila kusafiri umbali mrefu.
Kwa Upande Wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Dkt. Peter Kisenge amesema kwasasa Taasisi hiyo imeanza mchakato wa kufunga Mitambo ya kisasa ya matibabu, huku Madaktari Bingwa wakianza kuwasili kwenye Hospitali hizo Mbili, akisema wapo tayari kikamilifu kutekeleza maono ya Rais Dkt. Samia ya kutaka Utalii wa Matibabu utekelezwe Mkoani Arusha.