TUME YAWANOA MAAFISA WA POLISI KUELEKEA UCHAGUZI

0


Katika kuepusha nchi kuingia katika machafuko baada ya kufanyika uchaguzi na kuvipelekea vyombo vya ulinzi na usalama hususani Polisi kuanza kutuliza ghasia na kurejesha hali ya utulivu na amani, Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi imewanoa Wakuu wa Upelelezi wa Wilaya na Vikosi nchini, kuhusu sheria za Uchaguzi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku moja kwa maafisa hao wa Jeshi la Polisi nchini, Mkurugenzi wa uchaguzi kutoka Tume, Bw. Kailima Ramadhani amesema wameamua kulijengea uwezo Jeshi la Polisi ili waweze kutambua matakwa ya sheria za uchaguzi na kuepusha kuyumbishwa na wanasiasa.

“Mtakapokuwa mnachukua hatua za kulinda usalama katika vipindi hivi muwe na uelewa haki za vyama, wananchi na makundi mengine katika vipindi vyote, kwa maana wakati huu wa maandalizi ya kuelekea uchaguzi Mkuu, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi,”alisema Kailima.

Aidha, Kailima amesema ni vyemna maafisa hao wa Polisi wakawa na utamaduni wa kujikumbusha sheria mbalimbali ikiwemo zinazohusu masuala ya uchaguzi ili kuepuka kuyumbishwa na wanasiasa wanaoamua kupotosha yaliyomo katika sheria kwa maslahi yao binafsi.

“Mapitio yenu katika sheria yatawasaidia kutambua makosa yanayofanywa wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, uteuzi wa wagombea, wakati wa kampeni, wakati wa upigaji kura, kuhesabu na kujumlisha kura na wakati wa kutangaza matokeo,” alisema Kailima.

Alisema Mafunzo hayo kuhusu sheria za uchaguzi yana umuhimu na maana kubwa katika maandalizi ya zoezi zima na mchakato wa kuelekea chaguzi zilizopo mbele yetu kama Taifa,

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya Jinai CP Ramadhani Kingai ameshukuru uwepo wa semina hiyo kwani imewakumbusha wapelelezi kujua sheria, taratibu na miongozo inayosimamia chaguzi zinazo simamiwa na tume ya uchaguzi Tanzania

Mbali na mafunzo kuhusu sheria za uchaguzi pia maafisa hao wamepata fursa ya kukumbushwa masuala mbalimbali ikiwemo wajibu wa Jeshi la Polisi wakati wa ukaguzi, Bank Note Security features, utambuzi wa bidhaa bandia na hati miliki, upelelezi sambamba na utafiti katika mapungufu ya kisheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *