TMDA YAIPONGEZA NHC KWA UJENZI WA KIWANGO BORA NA KWA WAKATI DODOMA

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Erick Shitindi, ameipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kukamilisha ujenzi wa jengo la TMDA kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu. Shitindi alitoa pongezi hizo katika hafla fupi ya makabidhiano ya jengo hilo, iliyofanyika Dodoma, huku akishuhudiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo, pamoja na watendaji mbalimbali kutoka pande zote.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwenyekiti Shitindi alieleza kuwa licha ya NHC kuwa na miradi mingi inayotekelezwa kwa sasa, imeweza kutimiza wajibu wake wa ujenzi wa mradi huo wa TMDA kwa wakati, hatua ambayo imepokelewa kwa shukrani kubwa na mamlaka hiyo. Aliisifu NHC kwa kujenga jengo hilo kwa viwango vya juu, jambo ambalo linaashiria ubora wa kazi na usimamizi thabiti wa Shirika hilo.

“Shirika la Nyumba la Taifa lina miradi mingi ya ujenzi kote nchini, lakini liliweza kuhakikisha jengo letu linakamilika kwa wakati. Tunawashukuru sana kwa kazi hii nzuri na kwa kuzingatia ubora uliokusudiwa,” alisema Shitindi huku akiipongeza timu nzima ya NHC kwa juhudi zao.
Naye Meneja wa NHC wa mkoa wa Dodoma, Bw. Gibson Mwaigomole, alitoa shukrani kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NHC na Menejimenti kwa ujumla. Alisema Shirika la Nyumba la Taifa linajivunia sana kutekeleza mradi huo wa TMDA kwa ufanisi mkubwa, na kwa wakati kama ilivyohitajika. Mwaigomole aliongeza kuwa, mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya NHC na TMDA, na walijitahidi kuhakikisha wanakidhi matarajio ya wateja wao.
“Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba ilituamini na kutupa jukumu hili muhimu, na kwa niaba ya Shirika na uongozi kwa ujumla, tunawashukuru kwa kutupa fursa hiyo. Tumejizatiti kutoa huduma bora na tunajivunia mafanikio haya,” alisema Mwaigomole.
Hafla hiyo ya makabidhiano ilihudhuriwa na watendaji mbalimbali kutoka TMDA na NHC, na ilitawaliwa na shukrani na pongezi kwa ufanisi mkubwa wa Shirika la Nyumba la Taifa.