TANZANIA YA NNE UZALISHAJI DHAHABU AFRIKA -DKT. BITEKO

0

Tanzania inashika nafasi ya Nne kwa uzalishaji wa Madini ya Dhahabu Afrika lakini bahati mbaya haina akiba ya kutosha ya madini hayo Benki ambapo azma ya Serikali ni kuwa na hifadhi ya kutosha ya dhaha
bu katika Benki Kuu ya Tanzania.

Hayo ameyasema Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko Oktoba 04, 2024 wakati akifungua Maonesho ya Saba ya Kitaifa ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili Mkoani Geita.

“Tuna Madini Afrika nzima  nchi yetu ni ya nne lakini hatuna akiba ya dhahabu na nyingi tunapeleka mataifa mengine,” amesema Dkt Biteko na kuongeza “mfumo uliowekwa na Wizara hii, mnamazingira mazuri ya kufanya biashara kuliko wakati wowote ule kwenye historia, ungeni mkono juhudi za serikali, akiba ya dhahabu itatusaidia kuimarisha shilingi yetu wakati wa msukosuko unapotokea.

“Matatizo mbalimbali yanayotokea, Marekani wameamua kubadilisha Sera yao na wameitisha Dola zote kwenda kwao, sisi na nchi nyingine za Kiafrika tunahaha kupata Dola, utajiri tulionao ni dhahabu lakini hatua akiba,” amesema Dkt. Biteko.

Aidha, ameipongeza Sekta ya Madini kwa kuimarisha  ukusanyaji wa mapato na  udhibiti wa mianya ya utoroshaji wa madini na kuwafanya wachimbaji wafanikiwe.

Pia, Dkt. Biteko ametoa wito kwa wananchi kutembelea mabanda mbalimbali katika Maonesho hayo ili kujifunza masula mbalimbali ikiwemo namna bora ya uchimbaji salama, utafiti, uchenjuaji, uongezaji thamani madini na biashara ya madini.

Amesema lengo la Maonesho hayo, ni kuwakutanisha Wawekezaji, wachimbaji, wafanyabiashara na wachenjuaji wa madini ili kujifunza shughuli za utafiti na mnyororo mzima wa uongezaji thamani Madini.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amempongeza Dkt. Biteko kwa kutenga muda wake na kuja kuungana katika ufunguzi wa Maonesho hayo na pia amempongeza Rais wa Tanzania kwa kuiongezea bajeti Wizara ya Madini kwa lengo la kuimarisha sekta hiyo ili iweze kuwahudumia wachimbaji, wachenjuaji na wafanyabiashara ya madini ili wachimbe kwa tija na kunufaisha wao pamoja na Taifa kwa ujumla.

Mavunde amesema, Mhe. Rais ameongeza bajeti ya Wizara ya Madini kutoka bilioni 89 mpaka shilingi bilioni 231 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 110.4 zimeelekezwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili kusaidia katika ujenzi wa maabara za kisasa na utafiti wa kina kwa lengo la kumsaidia mchimbaji kujua maeneo yenye madini, kiasi kilichopo na muelekeo wa miamba ya madini kwa lengo la kuepusha upotevu wa mitaji.

Pamoja na mambo mengine, Mavunde amesema hivi karibuni kulitokea mgomo wa wafanyabiasha wa Madini hawakuwa tayari kuridhia mabadiliko ya Sheria, baada ya kikao kufanyika na kukubaliana kimsingi, hakuna mfanyabiashara atakaegoma, BoT atauziwa dhahabu kwa bei ya soko la dunia na malipo yatalipwa ndani ya saa 24.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigella amesema, Serikali kupitia Wizara ya Madini na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita imekusudia kuyafanya Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini kuwa Maonesho ya Kimataifa ambapo kwa Mwaka 2024 zaidi ya washiriki 816 wameshiriki ukilinganisha na washiriki 317 walioshiriki Mwaka 2023.

Sambamba na hayo, Shigela amesema Mkoa wa Geita umetoa leseni kwa wachimbaji wadogo 3,000 kati ya hizo vikundi 20 vya wanawake ambao idadi yao ni zaidi ya 1,000 na pia Mkoa huo unazalisha dhahabu kilo 16,612  kila mwaka na kati ya  tani hizo kilo 5,000 ni za wachimbaji wadogo  pekee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *