SERIKALI KUONGEZA IDADI YA VIZIMBA ILI KUPUNGUZA CHANGAMOTO YA MAMBA KANDA YA ZIWA
Serikali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi yake ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA imetenga fedha zaidi ya shilingi milioni 210 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya ujenzi wa vizimba saba Kanda ya Ziwa ili kuwalinda wananchi dhidi ya athari za wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba.
Kauli hiyo imetolewa Oktoba 01, 2024 na Mkuu wa wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga Katika ziara ya kukagua miradi ya vizimba na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vizimba hivyo kwa wananchi wa Buchosa, ziara iliyofanywa na TAWA wilayani humo.
“Tunashukuru sana Kwa hii hatua ambayo imefanywa na Serikali ya kuongeza bajeti ya kujenga vizimba vingine, nimesikia bajeti hii tunayoendelea nayo imetengwa zaidi ya shilingi milioni 200 nyingine Kwa ajili ya kutengeneza vizimba zaidi ya saba ” amesema Mhe. Senyi
Mhe. Senyi pia amepongeza jitahada zinazofanywa na TAWA katika kudhibiti wanyamapori hao, kutoa elimu Kwa wananchi pamoja na mwitikio wa haraka pale wananchi wanapohitaji msaada wao.
“Tunawashukuru sana wenzetu wa TAWA kwasababu tumeona matukio yanapungua Kwa kiasi kikubwa hasa Kwenye yale maeneo ambayo tayari tumeshaweka vizimba, lakini pamoja na vizimba watu wa TAWA wanatoa elimu, kwahiyo unaona maeneo ambayo hakuna vizimba elimu inawasaidia sana” amesisitiza Mhe. Senyi.
Naye Afisa uhifadhi II kutoka Kituo kidogo cha Kanda ya Ziwa Mwanza, Mohamed Mpoto amesema katika kipindi cha miezi miwili kuanzia Julai – Septemba, 2024 jumla ya watu 1,523 kutoka vijiji vitano (Izindabo, Nyonga, Lugata, Nyachitare na Kahunda) vya Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema waliweza kufiwa na elimu ya kuepuka madhara yanaweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko, elimu iliyotolewa na Maofisa wa TAWA Kwa njia ya mikutano ya hadhara.
Kwa upande wake Afisa habari wa TAWA Beatus Maganja amebainisha maeneo ambayo vizimba hivyo vitajengwa kuwa ni pamoja na vijiji vya Izindabo na Nyakasasa (Buchosa), Chinfunfu (Sengerema) na vijiji vya Kasahunga, Iramba, Butimba na Nerumba vilivyoko wilaya ya Bunda.
Ongezeko la idadi ya vizimba hivyo litaifanya Halmashauri ya Buchosa kuwa na jumla ya vizimba sita, idadi inayotajwa kuwa ni kubwa kuliko sehemu zingine zote zilizojengwa vizimba nchini.
Aidha Maganja amewasisitiza wananchi wa wilaya ya Sengerema hususani Halmashauri ya Buchosa kuwa na matumizi sahihi ya vizimba hivyo ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao sambamba na kuchukua tahadhari wanapokuwa wakifanya shughuli mbalimbali za kiuchumi katika ziwa Victoria.
Kufuatia hatua hiyo, wananchi wa Buchosa wameishukuru Serikali kwa jitihada na hatua mbalimbali inazozichukua Kwa ajili ya kuokoa maisha yao kwa kuwajengea vizimba ambayo wanakiri kuwa vimekuwa na msaada mkubwa kwao.