WAZIRI MWIGULU ATOA MAAGIZO KWA BODI YA WAKURUGENZI PPRA

0

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), ameiagiza kuiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kuhakikisha kuwa watoa huduma wanaopata zabuni kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Kieletroniki wa NeST, wanatumia malighafi na bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi isipokuwa kwa bidhaa ambazo ni lazima ziagizwe nje ya nchi kutokana na kutopatikana hapa nchini.

Dkt. Nchemba, amepokea maelekezo hayo wakati akipokea Taarifa ya Tathmini ya Utendaji Kazi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kwa mwaka wa fedha 2023/2024, tukio lililofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha Jijini Dar es Salaam, 28 Septemba, 2024.

Dkt. Nchemba alisema kuwa na, hatua itakuza uzalishaji wa bidhaa na huduma za ndani, kukuza ajira, kuongeza wigo wa kodi na kuchangia maendeleo ya nchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali.

Aidha, Dkt. Nchemba amezitaka Taasisi za umma nchini kuhakikisha zinatumia Mfumo wa Ununuzi wa Umma wa Kielektroniki (NeST) kwakuwa hakuna mbadala wake.

Alisema kuwa matumizi ya Mfumo wa Ununuzi wa NeST unaongeza uwazi na uwajibikaji na udhibiti wa ndani wa Taasisi nunuzi, na hivyo kuendana na maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyeitaka Wizara ya Fedha kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali hasa kwenye utekelezaji wa miradi ili iendane na thamani ya fedha inayotumika kutekeleza miradi husika.

Akizungumza wakati wa kukabidhi Taarifa hiyo ya Tathimini ya Utekelezaji wa Majukumu ya PPRA kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka hiyo, Dkt. Leonada Mwagike, alisema kuwa Taasisi yake inajivunia mafanikio makubwa ikiwemo kufanikisha maboresho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 na kanuni zake za Mwaka 2024.

Alisema kuwa katika kutekeleza majukumu yake ya ukaguzi na usimamizi wa Sheria za Ununuzi wa Umma, PPRA ilifanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 14.94 kupitia ukaguzi na kiasi kingine cha shilingi trilioni 2.7 wakati wa ufuatiliaji wa mipango kazi ya Ununuzi wa Taasisi Nunuzi iliyowasilishwa katika Taasisi hiyo na kubainika kuwa matumizi hayo hayakuwa na tija.

Aidha, alisema kuwa PPRA iliwezesha ushiriki wa Makundi Maalum, yakiwemo ya wanawake, vijana, watu wenye mahitaji maalum, kunufaika na zabuni 153 zenye thamani ya shilingi bilioni 5.29.

Ripoti hiyo imekabidhiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, Dkt. Leonada Mwagike na kushuhudiwa na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo na Bi. Amina Khamis Shaaban, Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, baadhi ya Menejimenti ya Wizara ya Fedha, wafanyakazi wa PPRA na wageni wengine waalikwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *