ASKOFU BAGONZA ATAMBUA KAZI NZURI YA TARURA

0


•Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa aipongeza TARURA Manunuzi Kidigitali/kielektroniki

Karagwe

Askofu wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Karagwe, Dkt. Benson Bagonza ameipongeza serikali kwa kuhakikisha inarudisha kodi za wananchi kwa kutekeleza miradi ya kisasa ya barabara.

Dkt. Bagoza ametoa pongezi hizo leo katika uzinduzi wa barabara ya lami yenye mita 700 Kishao -Lukajange ambapo amesema serikali imeendelea kuwa na uaminifu wa kukusanya fedha za wananchi na kuzirudisha katika jamii kwa kutekeleza miradi imara ikiwemo  barabara nzuri.

Amesema barabara hiyo ambayo inaelekea katika makao makuu ya Dayosisi ya Karagwe imekuwa kiunganishi  kikubwa kati ya wananchi na waumini na kuondoa vikwazo kwa wanachi ambao zamani walishindwa kuhudhuria ibada kwa kisingizio cha matope.

“Kazi kubwa ya Mwenge wa Uhuru ni kumulika miradi na kuzindua naungana na kila mtu kutambua kazi kubwa ya Tarura, wanafanya kazi nzuri, miradi ya viwango, ombi langu kwa serikali ni kuwa Mwenge wa Uhuru kwa sasa umulike maaadui wetu tulionao ndani ya nchi,”amesema Bagonza.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey Mnzava akipongeza hatua za manunuzi zilizofanywa na Tarura kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo huku amesema mfumo wa manunuzi wa kidigitali/kielektroniki umepunguza mianya ya rushwa na kuweka wazi wazabuni wenye sifa za kutekeleza miradi ya barabara.

Meneja wa Tarura Wilaya ya Karagwe, Mhandisi Kalimbula Malimi amesema mradi huo umetekelezwa kwa thamani ya Sh milioni 385 lengo likiwa kuboresha huduma za kiuchumi kwa wananchi na kupendezesha  eneo la mjini huku chanzo cha fedha hizo ikiwa ni tozo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *