WAZIRI JAFO:TUTAENDELEA KUFUFUA NA KUANZISHA VIWANDA VIPYA LINDI

0

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo, amesema wizara itaendelea kutafuta Wawekezaji Sahihi wenye nia ya kuanzisha viwanda vipya na kufufua vilivyosimama ikiwamo vya kubangua korosho mkoani Lindi ili kukuza uchumi na kuongeza fursa za ajira.

Dkt. Jafo ameyasema hayo alipokuwa, akihitimisha ziara ya siku sita mkoani humo yenye kauli mbiu isemayo ‘Rais Samia na Maendeleo Wasikie na Waone’ inayolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na Mkoa wa Lindi itatafuta wawekezaji hao ili kukuza biashara, Pato la Taifa na uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Pamoja na hayo, Waziri Jafo alisisitiza wananchi wa Mkoa huo kujiunga na kutumia vyama vya ushirika, kuhifadhi mazao yenye ubora kwenya ghala zinazotumia Mfumo wa Stakabadhi Za Ghala ili kuongeza thamani ya mazao na kuepuka uchakachuji utakaosababisha wakose soko na kuchafua taswira ya nchi ya Tanzania.

“Niwahakikishie wafanyabiashara wa Mkoa huu Serikali ya Awamu ya Sita itaendele kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji kutokana na kuwa na mazingira na miundombinu mizuri inayochochea uwekezaji ikiwamo miundombinu ya barabara, reli ya kisasa (SGR), maji na umeme,”amesema

Akiweka Jiwe la Msingi katika Miradi mbalimbali ya Maendeleo katika sekta ya afya, elimu, maji, ujenzi, uzalishaji pamoja na kuongea na Wananchi wakati wa ziara hiyo, Waziri Jafo amesema Mkoa wa Lindi umetekeleza miradi hiyo kwa ufanisi na kuutaka kuendelea kusimamia miradi ambayo haijakamilika ikamilike kwa wakati na ianze kutoa huduma kwa umma.

Aidha, Waziri Jafo, amewasisitiza Wananchi wa Mkoa huo kuhakikisha wanawapeleka watoto wote wenye mahitaji maalum katika shule zilizojengwa kwa ajili yao ili wapate elimu kama haki yao ya msingi ya kijamii.

Kadhalika, Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Bi Zuwena Omary na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Victoria Mwanziva wameishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo Mkoani humo na kuahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi katika muda uliopangwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *