MACHIFU WAKEMEA WANAOCHOCHEA UVUNJIFU WA AMANI
Na Mwandishi Wetu, RUVUMA
MACHIFU wa makabila mbalimbali nchini wametoa tamko la kuwaomba watanzania kutokubali kuvuruga amani iliyopo na kumheshimu Rais Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuwaletea maendeleo.
Aidha, wamemshukuru Rais Samia kwa kutambua umuhimu wao na kuahidi kuendelea kuombea uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani ili Tanzania iendelee kuwa na amani.
Wakizungumza mjini Songea kwenye mjadala kuhusu mstakabali wa Tanzania kwenye masuala ya mila na desturi ikiwa ni sehemu ya Tamasha la Kitaifa la tatu la Utamaduni Mwenyekiti wa Machifu Tanzania, Chifu Antonia Matalu alisema wamejadili masuala mbalimbali ikiwamo namna Rais Samia anavyowajali na kutambua umuhimu wao kwa jamii na kukemea watanzania wanaomdharau na kutishia kufanya maandamano.
“Machifu tutamlinda Rais wetu kwa gharama yoyote kwasababu tunampenda, amehimiza mila na tamaduni zetu kuheshimiana, Rais wetu ni zawadi kwetu,”alisema.
Alisema Rais amewapa majukumu ya kushikamana na raia kwa maendeleo ya Tanzania.
“Tunamuamini mama ni jasiri na tunaimani naye nchi hii anaiendesha vizuri, hapa machifu tumezungumzia maadili Rais aheshimiwe na tunakemea wale wanamdharau waache mara moja,”alisema.
Alisema Machifu wanapenda amani na wanasisitiza watanzania wailinde na kuitunza.
“Tumeshuhudia nchi nyingi zikipigana na sisi tukipokea wakimbizi, sisi tuna Rais mama mwenye huruma hata wale waliokimbia aliwaambia warudi watoto wangu mrudi nyumbani mnataka nini, tumpe mama yetu amani, msaada viongozi wote tushikamane naye kumpa faraja maana anatukanwa kwa ajili ya watanzania,”alisema.
Alisema Tanzania ni tulivu na sio watu wa maandamano na nchi zingine zimekuwa zikitamani amani iliyopo.
“Sisi sio watu wa maandamano hata kidogo, tunaomba Rais aheshimiwe, Machifu hapa tunasema Rais aheshimiwe,”alisema.
WAJADILI MAADILI
Machifu hao walisema pamoja na viongozi wa mila na desturi kuwa dini zao lakini pia wana maombi yao ya asili ni muhimu kuombea uchaguzi ufanyike kwa amani.
Dada wa wa Chifu Adam II, Fatma Mkwawa alisema “Tuombee uchaguzi na Rais wetu Samia Suluhu Hassan aendelee kutuongoza kwa kuwa mama halali kwa ajili yetu, tutamuombea. Niwaombe viongozi wa kimila ambao ni vijana mpate muda wa kuzungumza na vijana wenzenu.”
Aidha, alisema suala la maadili linapaswa kufuatiliwa kwa karibu na viongozi wa kimila na kutoa msaada kwenye makuzi ya watoto hasa wanaojilea wenyewe bila wazazi.
“Masuala ya ukatili wa kijinsia, mapenzi ya jinsia moja hayatakuwepo,”alisema.
Alihimiza vijana kutunza amani, mila na desturi na kujiepusha na mapenzi ya jinsia moja zilizopo ili Tanzania iendelee kupiga hatua za kimaendeleo
Chifu Songea Mbano 1, Samweli alimshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ya kushirikisha viongozi wa kimila na kuomba elimu endelee kutolewa vijana watambue machifu sio wachawi ni watu wa mila na desturi.
Aliomba umoja, amani, ushirikiano udumu kwa machifu nchini na kulinda mila na desturi.
Chifu Kasusula alikemea tabia ya jamii kutengeneza matukio ya uchonganishi yanayosababisha watu kujishughulikia sheria mkononi na kusababisha madhara kwa jamii.
Msaidizi wa Chifu Masanja kutoka Bunda, Lucia alisema kuna tatizo la mmonyoko wa maadili kwenye jamii na kuwaomba machifu kukemea vitendo hivyo.
“Nimshukuru Rais kwa kutambua umuhimu wa Machifu naomba tuendelee kufanya kazi hii kwa uaminifu ili taifa lisonge mbele,”alisema.
Kadhalika, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed alisema machifu wana umuhimu mkubwa nchini na kuwaomba kumuombea Rais Samia.
MWISHO