MAMA MARIAM MWINYI AWASILI MAREKANI KUSHIRIKI MIKUTANO YA OAFLAD
Mke wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mhe. Mama Mariam Mwinyi, ameondoka Zanzibar na kuwasili New York, Marekani, tarehe 20 Septemba 2024, kuiwakilisha Tanzania katika mikutano iliyoandaliwa na Taasisi ya Wake wa Marais Barani Afrika (OAFLAD), itakayofanyika New York kuanzia Septemba 21 hadi Septemba 26, 2024.
Mkutano huo utajadili uwekezaji na utekelezaji wa afua jumuishi za kijamii, hususan afya na elimu kwa watoto na wasichana.
Aidha Mikutano hiyo itafanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA), ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mama Mariam Mwinyi amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Elsi Kanza, pamoja na Balozi Dkt. Suleiman Haji Suleiman, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa John F. Kennedy.