WAZIRI OR – TAMISEMI ATANGAZA MAJINA YA MIPAKA YA MITAA, VIJIJI NA VITONGOJI.

0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Omar Mchengerwa ametangaza rasmi Majina ya Mipaka ya Mitaa,Vijiji na Vitongoji Nchini, kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.

Mheshimiwa Mchengerwa ametangaza notisi ya mgawanyo ya maeneo ya Utawala katika Mamlaka za Miji, Majiji, Manispaa na wilaya ambapo notisi hiyo imeainisha jumla ya Vijiji 12,332, Mitaa 4,269 na vitongoji 64, 74 kushiriki kwenye uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa.

Waziri Mchengerwa ametangaza majina hayo ya mipka akiwa Mkoani Arusha, leo tarehe 16 Septemba 2024, na kusema kuwa, amri ya Mgawanyo wa Maeneo ya Utawala katika Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) (Tangazo la Serikali Na. 796 la mwaka 2024) imetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 30 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287.

Notisi ya Mgawanyo wa Maeneo ya Utawala katika Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) (Tangazo la Serikali Na. 797 la mwaka 2024) imetolewa kwa mujibu wa vifungu vya 16(1) na 18(1) vya Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288.

Aidha, amefafanua kuwa, matangazo hayo yamejumuisha maeneo yaliyokuwa yamefutwa awali kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 673 na 674, ambayo yalihusisha pia Tarafa ya Ngorongoro.

“Lengo la hatua hii ni kuhakikisha kuwa maeneo haya yanapata uwakilishi mzuri wa kiutawala, pamoja na huduma za kijamii na kiuchumi zinazowiana na mahitaji ya wananchi wake” Amesema

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *