NINYI YOTE NI NDUGU, KATIBU MKUU WA TEC PADRI DKT. KITIMA
Katibu Mkuu wa TEC Padri Dkt. Charles Kitima amewaita na kuwasimamisha pamoja kisha kuwatambulisha kwa Waumini, Katibu Mkuu wa CCM, Emmanuel Nchimbi, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA- Bara, Tundu Lissu na Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika na kisha kumuelezea kila mmoja kwa ufupi ambapo pamoja na mengine katika kuwaelezea kwake, Padri Kitima ametumia muda mwingi kurejea maneno “Ninyi nyote ni Ndugu, mkaishi kwa upendo” na amewataka wapeleke tunu za Injili na wakasambaze upendo kwenye Vyama vya Siasa.
Hayo yamejiri leo Jumapili September 15,2024 kwenye uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam ambako kunafanyika kilele cha kongamano la 5 la Ekaristi Takatifu Kitaifa ambapo maelfu ya waumini wa Kanisa Katoliki Nchini wanashiriki wakiongozwa na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Wolfgang Pisa.
Padri Kitima amesema “Kuna siku mwaka 2017 nilienda Nairobi kumsalimia Mgonjwa kutoka Jimbo la Singida (Tundu Lissu) ambaye alikuwa amepigwa risasi kwasababu ambazo mpala leo hatuzijui, nikaenda nikamkuta amelala nikamwambia weee Mheshimiwa pole akasema asante Father lakini alikuwa anaongea Kinyaturu sasa nikamwambia utamsemehe aliyekupiga risasi akaniuliza namsameheje wakati simjui?, nioneshe, lakini kwa Kinyaturu akaniambia Father Mungu yupo nimeshuhudia uwepo wake, huyo ni Lissu sitompa aongee sababu najua Wanasiasa wanaweza wakaanza kurushiana maneno hapahapa”
“Msisahau Nchimbi amesoma na Baba Urasa Uru Seminary kwahiyo maadili ya Seminary lazima yaingie huko, Mnyika alikuwa anataka kuwa kama Father Ruwa’ichi na amechelewa kweli kuoa, Mnyika ameoa mwaka huu unaweza ukaamini?, Mnyika nae alisoma Maua Seminary kwahiyo sala za Mtakatifu Francis zipo hapa, ndio maana hata siku ile Mbeya alipotaka kupigwa hajui kurusha ngumi anasema wananiua basi akaokoka, nyinyi nyote ni Ndugu pelekeni tunu za Injili kwenye Vyama vya Siasa”