CCM YAANZA MAZUNGUMZO NA VYAMA VYA UPINZANI

0

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kinaendelea na mazungumzo yasiyo rasmi na vyama vya upinzani ili kujenga mwafaka wa pamoja.

Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema ni lazima kujenga mwafaka wa pamoja na kwamba wakati utakapofika wataweka hadharani mkakati wa mazungumzo hayo.

Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali nchini kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba mkoani Dar es Salaam, Dkt. Nchimbi ameongeza kuwa tayari ameanza mazungumzo na Katibu Mkuu mwenzake wa Chama cha ACT – Wazalendo yanayolenga maridhiano.

Msingi wa mwafaka huo wa pamoja, amesema ni kuzingatia kwa mapana yake falsafa ya R4 ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan inayosisitiza maridhiano.

Falsafa ya R4 inahusisha; maridhiano, ustahimilivu, mageuzi, na ujenzi mpya wa nchi. Ni falsafa inayolenga kushughulikia changamoto za kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini huku ikijenga mazingira ya ushirikishwaji na demokrasia.

Kupitia maridhiano, uongozi wa Rais Samia amefanya juhudi za kuondoa mgawanyiko wa kisiasa kwa kurudisha mikutano ya hadhara na kuzungumza na viongozi wa upinzani. Kwa ujumla, mkakati wa 4R ni nia njema ya Rais Samia katika kukuza umoja, kuboresha ushirikishwaji wa kidemokrasia, na kuhakikisha ukuaji endelevu wa uchumi nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *