REA YAENDELEA KUTEKELEZA KWA VITENDO MKAKATI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatarajia kusaini mikataba yenye thamani ya shilingi bilioni 50.98 kwa ajili ya kuhamasisha umma kuachana na matumizi ya nishati za kupikia zisizo salama ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi za Kupikia.
Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage amebainisha hayo katika mkutano na Waandishi wa Habari Septemba 11, 2024 Jijini Dodoma.
Alisema utekelezaji wa miradi ya Nishati Safi na Zilizoboreshwa za Kupikia ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi 2024- 2034 ambao unaelekeza ifikapo Mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi za kupikia.
“Hivi karibuni, Wakala utasaini mikataba kadhaa ya ushirikiano na wadau mbalimbali ambayo yote kwa pamoja imelenga kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi za Kupikia kwa wote kama Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati safi za Kupikia unavyoelekeza,” alifafanua Mhandisi Advera.
Mhandisi Advera alisema Wakala umefikia makubaliano ya ushirikiano wa utekelezaji wa miradi ya kujenga na kusambaza mifumo ya Nishati safi za Kupikia na Jeshi la Magereza pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambapo mifumo mbalimbali ya nishati safi na iliyoboreshwa itafungwa katika taasisi hizo.
Alisema kwa upande wa Jeshi la Magereza (TPS), mikataba itakayosainiwa ina thamani ya shilingi bilioni 35.23 ambapo kati ya fedha hizo 75.5% ambayo ni sawa na shilingi bilioni 26.57 zitatolewa na REA na 24.6% sawa na shilingi bilioni 8.66 zitatolewa na Jeshi la Magereza kwa Mradi utakaotekelezwa kwa muda wa miaka mitatu katika Magereza 129 yaliyopo Tanzania Bara.
“Katika mkataba huu na Magereza kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa mifumo ya bayogesi (gesi vunde) 126, usimikaji wa mifumo 64 ya gesi ya LPG, usimikaji wa mfumo wa gesi asilia, usambazaji wa mitungi ya gesi (LPG) ya kilo 15 ikiwa na jiko la sahani mbili ipatayo 15,920 kwa watumishi wa Magereza, usambazaji wa tani 865 za mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe kutoka STAMICO,” alifafanua Mhandisi Advera.
Alisema mkataba huo wa Magereza vilevile utahusisha pia usambazaji wa mashine 61 za kutengeneza mkaa mbadala, ujengaji uwezo kwa watumishi 280 wa Jeshi la Magereza na usambazaji wa majiko banifu 977 ambapo kati ya majiko hayo, 377 yatatumia nishati ya bayogesi, 256 yatatumia LPG na 344 yatatumia nishati ya mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe kwa kuanzia na baadaye kwa mkaa unaotokana na mabaki ya mazao mbalimbali.
Aidha, kwa upande wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), alisema mikataba itakayosainiwa ina thamani ya shilingi bilioni 5.75 ambapo kati ya fedha hizo 76% ambayo ni sawa na shilingi bilioni 4.36 itatolewa na REA na huku 24% sawa na shilingi bilioni 1.39 itatolewa na JKT.
“Fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi katika Kambi 22 za JKT kwa muda wa miaka miwili itakayohusisha ujenzi wa mitambo 9 ya bayogesi, majiko 291 ya kutumia mkaa mbadala (makaa ya mawe na tungamotaka), ujenzi wa mifumo 180 ya kupikia inayotumia LPG na sufuria zake, ununuzi wa tani 110 za mkaa unaotokana na makaa ya mawe, ununuzi wa mashine 60 za kutengeneza mkaa mbadala na mafunzo kwa vijana wapatao 50,000,” alisema.
Mhandisi Advera alisema katika kuwezesha kaya za vijijini na zile zilizopo katika maeneo ya vijiji-miji kutumia nishati safi za kupikia na zilizoboreshwa, Serikali kupitia REA inaendelea kutoa ruzuku katika uuzaji wa wa mitungi ya gesi (LPG) ya Kilo 6.
Alizitaja kampuni zilizoshinda zabuni ya kusambaza mitungi hiyo kuwa ni Taifa Gas, Manjis, Oryx pamoja na Lake Oil ambapo alisema jumla ya mitungi 452,445 itasambazwa kwa bei ya ruzuku katika mikoa yote ya Tanzania Bara na huku kila wilaya ikinufaika na mitungi 3,255.