TAMASHA LA TATU LA UTAMADUNI LA KITAIFA KUFANYIKA MKOANI RUVUMA

0

Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inawaletea watanzania Tamasha la tatu la Utamaduni la Kitaifa, ambalo litafanyika Mkoani Ruvuma, Manispaa ya Songea kuanzia tarehe 20 hadi 23, Septemba 2024. Tamasha hili litafunguliwa na Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Septemba 20, 2024. Aidha, kilele cha tamasha hili tarehe 23 Septemba, 2024, mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Madhumuni ya tamasha hili ni pamoja na; kuenzi na kulinda utamaduni wetu, kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia ukuzaji wa sekta za ubunifu na utamaduni, kutoa jukwaa la kuonyesha utamaduni kama msukumo madhubuti wa utangamano wa kitaifa kwa kuwaleta/kuwaunganisha pamoja wadau na viongozi wa sekta, kuendeleza na kuenzi urithi wa utamaduni wetu, kutoa fursa ya majadiliano ya kitaaluma baina ya wananchi wa kila mkoa, kutumia utamaduni na ubunifu kama nyenzo ya kuenzi na kukuza utambulisho wa Taifa na kutangaza fursa na rasilimali za kipekee ilizonazo nchi yetu.

Kutokana na umuhimu na mvuto wa tamasha hili, naomba na kuwahakikishia kampuni zote, mashirika, asasi na taasisi zinazotoa huduma mbalimbali, washirika wa maendeleo na wadau kwa ujumla kujitokeza kudhamini tamasha hili.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo mahususi ya kufungamanisha utamaduni na utalii, utamaduni na biashara, utamaduni na uchumi kwa ujumla.

Kwa ujumla, tamasha hili ni fursa muhimu katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kisayansi, kisiasa na kiutamaduni. Aidha, ni njia mahususi ya kukuza viwanda vya ubunifu sanaa na utamaduni nchini.

Tamasha linaandaliwa katika namna ya kuzitangaza tunu zetu, vivutio vyetu vya kiutamaduni, tunaomba sana ushirikiano wa watanzania wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *