MZEE BUTIKU AFUNGUKA SAKATA LA WATU KUTEKWA “WANAJULIKANA”

0

Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mzee Joseph Butiku amesema Wahalifu wanaofanya vitendo vya utekaji na mauaji wanajulikana na kwamba wengine wamo hadi kwenye Vyombo vya Dola huku akiwataka Wananchi kushirikiana na Serikali kuwafichua na wanapobainika wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Akiongea na Waandishi wa Habari leo September 10,2024, Mzee Butiku amesema “Sisi Watanzania ni Wastaarabu, tusiseme hatuwajuwi Wahalifu hawa (wanaofanya mauaji na utekaji) ukweli ni kwamba tunawajua, wanaishi miongoni mwetu na katika kaya zetu, wapo ndani ya Vyombo vyetu vya dola, wapo Makanisani na Misikitini, narudia tena tunawajua na hapa ni lazima Serikali yetu iwajuwe”

“Taasisi ya Mwl Nyerere inaomba tumsaidie Rais Samia kupata taarifa sahihi kuhusu wabaya wetu hawa ili achukue hatua stahiki, anavyo Vyombo vya Dola vyenye majukumu mahsusi ya kumpatia taarifa za uhakika, Nchi yetu imeviwezesha Vyombo hivyo kuwa na uwezo wa kutosha wa utaalamu na uwezo wa vitendea kazi, Viongozi wa Vyombo hivyo wasituambie kwamba hawajuwi kinachotokea, wanajua, wasituambie kwamba wanamuogopa Rais, wasimsingizie, wote tumsaidie Rais wetu, tusiogope”

“Vyombo vya usalama ni Binadamu tu kama wewe Mwandishi na huenda miongoni mwetu humu wapo wengine kwasababu usalama ni Watu wengi, kila Mtanzania kwa mujibu wa Katiba yetu ni Mtu wa kuhakikisha kwamba Taifa hili linalindwa, Vyombo vya usalama ni Watu kama sisi, la kwanza kabisa si wote lakini wamo wachache wanaofanya hivyo (vitendo vya uhalifu kama uuaji na utekaji) lakini tunachosema kuhusu Vyombo vya usalama ni kwamba lazima wawajibike hasa Viongozi wao”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *