MAWAZIRI WA TANZANIA NA KOREA WAKUTANA, KUSHIRIKIANA KATIKA UJENZI WA MIUNDOMBINU.

0

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb) wamekutana na kuzungumza na Waziri wa Ardhi, Ujenzi na Uchukuzi wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Park Sang-Woo, leo tarehe 10 Septemba 2024 jijini Seoul, Korea Kusini.

Mazungumzo yamefanyika mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano wa Miundombinu kati ya Afrika na Jamhuri ya Korea (Global Infastructure Cooperation Conference – GICC 2024) unaofanyika nchini Korea Kusini kuanzia tarehe 12- 14, Septemba 2024.

Mawaziri hao wamejadili Masuala mbalimbali ya Ushirikiano ambapo Korea imekubali kushirikiana na Tanzania katika miradi ya kupunguza msongamano katika miji na majiji, kupima na kupanga maeneo ya miji pamoja na utekelezaji wa miundombinu mbalimbali.

Serikali ya Jamhuri ya Tanzania inashiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano wa Miundombinu kati ya Afrika na Jamhuri ya Korea (GICC 2024) ambapo ujumbe wa Mawaziri umeambatana na Wakuu wa Taasisi na Wataalam kutoka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Shirika la Reli Tanzania (TRC), Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo ni fursa ya kuimarisha ushirikiano, kupata na kubadilishana maarifa na uzoefu kutoka kwa nchi nyingine zitakazoshiriki pamoja na kukutana na Makampuni, Taasisi na Wataalam wa Jamhuri ya Korea ukizingatia nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika Sekta ya Miundombinu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *