JESHI LA ISRAELI LIMEWAUA WAPALESTINA 40 NA KUWAJERUHI WENGINE 60
Jeshi la Israeli limewaua Wapalestina 40 na kuwajeruhi wengine 60 katika mashambulizi ya anga kwenye kambi ya hema huko Khan Younis kusini mwa Gaza, madaktari walisema.
Afisa wa ulinzi wa raia wa Gaza ameliambia shirika la habari la AFP mapema Jumanne kwamba “mashahidi 40 na majeruhi 60 walipatikana na kuhamishiwa” katika hospitali za karibu kufuatia shambulio la Israel ndani ya eneo la kibinadamu la Al-Mawasi huko Khan Younis, mji mkuu wa kusini mwa eneo la Wapalestina.
Wakaazi na madaktari walisema kambi hiyo ya hema ilipigwa na angalau makombora manne ya Israeli. Kambi hiyo imejaa Wapalestina waliokimbia makazi yao ambao wamekimbia kutoka mahali pengine kwenye eneo hilo.
Huduma ya dharura ya raia wa Gaza ilisema takriban mahema 20 yaliteketea kwa moto, na makombora yalisababisha mashimo yenye kina cha futi 30.
“Timu zetu bado zinawahamisha mashahidi na waliojeruhiwa kutoka eneo lililolengwa. Inaonekana kama mauaji mapya ya Israel,” afisa wa dharura wa kiraia wa Gaza alisema.
Bila kutoa uthibitisho wowote, jeshi la Israel lilisema liliwashambulia wapiganaji wa Hamas ambao ilisema “walikuwa wamejikita ndani ya Eneo la Kibinadamu huko Khan Younis.”
Kundi la upinzani la Palestina Hamas lilikanusha kuwa wapiganaji wake walikuwepo katika eneo la mauaji ya Israel, likisema “Madai ya uvamizi wa [Israeli] ya kuwepo kwa wapiganaji wa upinzani ni uongo mtupu.”