FAMILIA YAOMBA UCHUNGUZI WA HARAKA KIFO CHA BABA YAO
Familia ya Mjumbe wa Sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Marehemu Ali Mohamed Kibao aliyezikwa jana jijini Tanga wameiomba serikali kuharakisha uchunguzi wa kifo cha baba yao ambae mwili wake ulipatikana maeneo ya Ununio jijini Dar es Salaam akiwa ameuawa baada ya kutekwa na watu wasiojulikana Septemba 6, 2024 katika maeneo ya Tegeta karibu na Jengo la Kibo Complex.
Wametoa ombi hilo mbele ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni baada ya Waziri huyo kufika nyumbani kwa marehemu jijini Tanga kutoa salamu za pole kwa niaba ya serikali ambapo pia aliwasilisha rambirambi ya kiasi cha shilingi milioni tano kwa niaba ya serikali.
Akizungumza mbele ya Waziri Masauni kwa niaba ya familia mtoto wa marehemu Ali Mohamed Kibao,Mariam Ali Mohamed ameiomba serikali kufanya uchunguzi wa kifo cha baba yao huku akiomba familia iwe inapatiwa taarifa za uchunguzi huo na isipite muda mrefu bila matokeo ya uchunguzi kutoka huku akiomba majibu ya uchunguzi yawafikie familia kwa njia rasmi na sio kusikia kupitia vyombo vya Habari.
‘Tumesikia Mheshimiwa Rais,Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza vyombo vya uchunguzi vifanye uchunguzi wa kifo cha baba yetu,sisi kama familia tutakua tunapataje taarifa za uchunguzi huo najua kuna muda inakua ni vigumu kuwafikia viongozi wa juu huko serikalini hasa kwa kesi kama hii ni jambo nzito,tunachoomba ni ushirikiano wenu kama serikali kwetu sisi maana hata sisi hatujui nani amefanya huo utekaji na mauaji ya baba yetu.Muhimu tunaomba huo uchunguzi ufanyike kwa haraka ili ukweli ujulikane na haki ipate kutendeka.’ Alisema Mariam
Akizungumza na familia ya marehemu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni aliwasilisha salamu za pole kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo ameiomba familia hiyo kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho wamempoteza mpendwa wao huku akiwaomba wawe na Subira ili vyombo husika vikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo la kutekwa na kuuawa kwa mzazi wao.
Marehemu Ali Mohamed Kibao ameacha wajane wawili na watoto kumi