CHADEMA WATAKA WAZIRI MASAUNI NA IGP WAMBURA WAJIUZULU
Viongozi wa CHADEMA akiwemo Katibu Mkuu, John Mnyika na Godbless Lema wametoa wito wa kumtaka Waziri wa Mambo ya Ndani , Injinia Hamad Masauni na IGP Camilius Wambura kuwajibika kwa kujiuzulu nafasi zao kutokana na matukio ya utekaji na mauaji ya Watu yanayoendelea Nchini.
Viongozi hao wametoa kauli hiyo leo September 09,2024 Mkoani Tanga wakati wa mazishi ya Kiongozi wa CHADEMA, Ali Kibao ambaye alitekwa na kuuawa Jijini Dar es salaam.
Lema amesema “Mtoto wangu analia, Mke wangu analia anahisi Mimi nipo kwenye list ya watakaouawa, Mh. Waziri nakuomba msiruhusu haya mambo, Mimi napita barabarani eti nikiona toyo nyuma yangu najua nimekuja kupigwa risasi, Mimi sijawahi kuwa na kesi ya jinai Nchi hii lakini natafutwa”
“Medy (Kibao) hajatekwa na Majambazi, ametekwa na Watu wa mfumo, mnatuumiza Waziri, nilitarajia baada ya statement ya Rais jana nilitarajia wewe uwe umejiuzulu, IGP awe amejiuzulu, jana tumeongea na Sugu zaidi ya saa moja namwambia naogopa kutoka ndani kwasababu natafutwa”
Kwa upande wake pia Katibu Mkuu Mnyika ameunga mkono kauli ya Lema akimtaka Masauni ajiuluzu “Kwa jinsi nilivyosikia Kondakta, Dereva na Abiria wa lile basi, Idara ya Usalama wa Taifa ndio Mtuhumiwa Mkuu”