UWT, WABUNGE KUFANYA TATHMINI ONGEZEKO LA MATUKIO YA UKATILI WA KIJINSIA
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Marry Chatanda, amezindua kampeni ya msaada wa Kisheria inayotekelezwa na Kamati ya Haki na Sheria ya UWT na kutaka ifanywe tathmini ya kina sababu zinazochangia kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kijinsia ili kuishauri serikali kudhibiti hali hiyo.
Chatanda kwenye hafla hiyo Septemba 7, 2024 jijini Dodoma, amesema tathmini hiyo ifanywe na kamati hiyo, wadau hiyo na wabunge watakaoteuliwa na ilenge kuangalia kama sheria inayotoa adhabu kwa wanaofanya ubakaji na ulawiti inahitaji marekebisho ili kuishauri serikali vifungu vya kurekebishwa vitakavyokuwa mwarobaini wa kuondokana na matukio hayo.
“Mtoto huyu anayebakwa kila siku atasoma? niwaombe tushirikiane katika jambo hili hakika linaumiza jamani viongozi wa Dodoma zungumzeni hili kuna shida gani mbona sisi wanawake watu wazima tupo wengi hata idadi ya wanawake walioolewa ni wachache kwanini mhangaike na watoto wadogo wambieni akina baba tupo kwanini wahangaike na watoto wadogo kwanini wahangaike na watoto wa miezi sita na kama mganga anasema nenda kambake mwanamke muulize mganga wako nikimpata hata mtu mzima dawa inawezekana njoo utukute sisi tupo barabarani,”amesema.
Akizungumza kuhusu kampeni hiyo, Chatanda amesema inaunga mkono jitihada za awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid Chini ya Wizara ya Katiba na Sheria inayofanya vizuri kwa sasa ili kutoa huduma za msaada wa kisheria na kuhakikisha upatikanaji wa haki sawa kwa wote kwa kuzingatia zaidi wanawake ,wasichana,watu wenye ulemavu na makundi mengine hatarishi.
“UWT inalenga kuchangia jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wote kuhusiana na matatizo ya ardhi,matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake urithi,Ndoa,kesi za madai na jinai,”amesema.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Naibu Waziri TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba amesema kwa awamu ya kwanza kampeni hiyo itafikia mikoa 10 na kila jumamosi ya mwisho wa mwezi kwenye ofisi za UWT kutakuwa na watoa msaada kisheria kutoka vyombo mbalimbali vya sheria.
Mhe.Katimba amesema kuwa Wanawake, watoto na watu wenye mahitaji maalum ndio walengwa kwenye kampeni hiyo na wameandaa program maalum kufikia watoto shuleni ili kupata elimu ya kujilinda na ukatili.
Amesema kuwa Rais Dkt.Samia aliona wananchi wanahitaji msaada ndio maana alianzisha kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia ambayo imekuwa na matokeo chanya.